Baraza la mawaziri Libya lafanyiwa mabadiliko.


Waziri Mkuu wa serikali ya maafikiano ya kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa amelifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri kwa kuteua mawaziri wanne wapya kushika nyadhifa za Wizara ya Mambo ya Ndani, Fedha, Uchumi na Viwanda na Vijana na Michezo.
Katika mabadiliko hayo, Waziri Mkuu Fayez al-Serraj amemteua Fathi Ali Bashagha kuwa waziri wa mambo ya ndani. Bashagha anatoka mji wa magharibi wa Misrata na yuko karibu na makundi yanayobeba silaha ya mji huo ambayo baadhi yao yalihusika na mapigano ya wiki kadhaa yaliyotokea katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Katika uteuzi huo mpya, Ali Abdulaziz Issawi ameteuliwa kuwa waziri wa uchumi na viwanda. Issawi anatoka mji wa Benghazi yaliko makao ya uongozi pinzani wa serikali ya Waziri Mkuu al-Serraj. Waziri huyo ni mmoja wa vinara wa waasi waliouangusha utawala wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.
Faraj Bomtari ameteuliwa kuwa waziri wa fedha na Bashir al-Qantri amekabidhiwa mamlaka ya kuongoza wizara ya vijana na michezo.
Wataalamu wa masuala ya Libya wameyatathmini mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri kama mkakati na juhudi za Waziri Mkuu wa serikali ya maafikiano ya kitaifa ya Libya ya kupanua wigo wa uungaji mkono wake kitaifa na kuimarisha usalama katika mji mkuu Tripoli.
Serikali ya maafikiano ya kitaifa ya Libya imekuwa ikitarajiwa kutangaza hatua kadhaa pia za kiusalama ikiwemo ya kuyataka makundi yenye silaha kuondoka kwenye majengo ya wizara na taasisi za serikali baada ya mapigano makali yaliyojiri hivi karibuni mjini Tripoli.

Leave a Comment