Waziri Mkuu wa Ethiopia afikia makubaliano na wanajeshi.


Abiy Ahmed Waziri Mkuu wa Ethiopia jana alifikia makubaliano na mamia kadhaa ya wanajeshi wa nchi hiyo waliofika ofisini kwake wakidai nyongeza ya mishahara; ambapo wanajeshi hao walikubaliwa kumuona Waziri Mkuu huyo.
Habari zinasema kuwa mkutano wa pande mbili hizo ulimalizika kwa kufikiwa makubaliano. Sambamba na kudai nyongeza ya mishahara, wanajeshi hao pia walimataka Waziri Mkuu wa Ethiopia kutazama upya muundo na oparesheni za jeshi la nchi hiyo.
Televisheni ya taifa haikuonyesha picha za wanajeshi hao waliofikia katika ofisi ya Waziri Mkuu hata hivyo watu walioshuhudia walisema kuwa mtandao wa intaneti ulizimwa kwa karibu masaa matatu jana mchana ili kuzuia kusambazwa taarifa za uwongo katika mitandao ya kijamii.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliye na umri wa miaka 42 ambaye aliingia madarakani mwezi Aprili mwaka huu baada ya nchi hiyo kughubikwa na machafuko kwa miaka kadhaa yaliyomlazimisha mtangulizi wake kujizulu ameahidi kufanya mabadiliko katika vikosi vya ulinzi na kuboresha demokrasia ya vyama vingi nchini humo.

Leave a Comment