Mafuriko Nigeria yauwa watu 199; mamia wakosa makazi.


Mafuriko yaliyoyaathiri maeneo mengi ya katikati na kusini mwa Nigeria yamesababisha vifo vya watu 199 hadi sasa. Hayo yameelezwa na Idara ya Kukabiliana na Majanga ya nchi hiyo.
Mafuriko ya mwaka huu nchini Nigeria yameathiri theluthi moja ya majimbo 36 ya nchi hiyo tangu mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu na kusibu watu milioni 1.92 na kuwafanya wengine 560,000 kukosa makazi. Msimu wa mvua nchini Nigeria unakaribia kumalizika hata hivyo maji yaliyosababishwa na mafuriko huenda yakachukua muda kukauka. Misaada ya kibinadamu inahitajika sasa huku nchi hiyo ikikabiliwa pia na kuenea maradhi ya kipindupindu.
Umoja wa Mataifa wiki iliyopita ulitangaza kuwa hadi sasa watu zaidi ya elfu tatu wamebainika kuugua kipindupindu na wenine 97 wameaga dunia katika majimbo ya Borno na Yobe kaskazini mashariki mwa Nigeria katika muda wa wiki mbili pekee zilizopita.
Mafuriko yaliyoikumba Nigeria katika miaka ya karibuni yamesababisha mamia ya maelfu ya raia nchini humo kukosa makazi.

Leave a Comment