Magaidi wa Boko Haram waua wanajeshi wanane Chad.


Shambulizi la wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram limeua wanajeshi 8 wa Chad katika eneo la Ziwa Chad katika shambulio ambalo lilijibiwa na wanajeshi hao na kuua wanamgambo 48.
Habari hiyo imethibitishwa na msemaji wa jeshi la Chad, Kaiga Kindji aliyesema kuwa, magaidi wa Boko Haram walishambulia maeneo ya jeshi la Chad mapema jana asubuhi.
Ameongeza kuwa, shambulizi hilo limejeruhi wanajeshi 11 wengine lakini limejibiwa vikali sana.
Chad ni mwanachama wa kikosi cha pamoja cha kupambana na Boko Haram katika mpaka wake na nchi tatu za Nigeria, Niger na Cameroon. Kikosi cha nchi hizo nne zinazopakana na Ziwa Chad kimeundwa kwa shabaha ya kuzuia mashambulizi ya genge hilo la wakufurishaji yasienee kutoka Nigeria hadi katika nchi hizo jirani.
Jeshi na serikali ya Nigeria inadai kuwa magaidi wa Boko Haram wamefurushwa katika sehemu kubwa ya ngome zao huko kaskazini mwa nchi hiyo.
Hata hivyo genge hilo bado linaendesha harakati zake katika msitu wa Sambisa huko Borno na limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na maafisa usalama wa serikali ya Nigeria kutokea msitu huo.
Zaidi ya watu 20,000 wameshauawa hadi hivi sasa mamia ya maelfu ya wengine wamekuwa wakimbizi tangu magaidi wa Boko Haram walipoanzisha mashambulizi yao nchini Nigeria miaka minane iliyopita na baadaye kupanua wigo wa mashambulizi yao hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon. Mwaka 2015 genge hilo lilitangaza utiifu wake kwa genge jingine la kigaidi la Daesh (ISIS).

Leave a Comment