UN yataka kufanyike uchunguzi wa haraka kuhusu jinai za Saudia nchini Yemen.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kufanyike uchunguzi wa haraka kuhusu jinai za hivi karibuni za muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia huko Yemen.
Mapema leo asubuhi, António Guterres amelaani jinai iliyofanywa jana na ndege za muungano wa Saudia zilizoshambulia basi lililokuwa na watoto wadogo mkoani Sa’ada, kaskazini mwa Yemen na kutaka uchunguzi wa haraka na huru ufanyike mara moja kuhusu jinai hiyo ya kutisha.
Jana usiku wizara ya afya ya Yemen ilisema kuwa, watu 50 wameuawa na 77 wengine wamejeruhiwa baada ya ndege za kivita za muungano vamizi unaoongozwa na Saudia kushambulia basi lililokuwa na watoto wadogo katika mji wa Dhahyan, mkoani Sa’ada.
Wizara ya Ulinzi ya Yemen jana usiku ilitoa tamko kuhusiana na jinai hiyo mpya ya Saudia na kusema kuwa jinai hiyo haitaachwa vivi hivi bila ya kujibiwa.
Taarifa ya wizara ya ulinzi ya Yemen imeongeza kuwa, wakati vikosi vya ulinzi vya Yemen vinaendesha mapambano ya kujihami kwa mujibu wa sheria za kimataifa, inaumiza kuona kuwa madola vamizi hasa Saudi Arabia, Imarati na vibaraka wao yanawashambulia kwa makusudi, watoto wadogo, wanawake na wanaume wasio na hatia huko Yemen.
Wizara za Mambo ya Nje za Iran na Syria zimelaani vikali jinai hiyo mpya ya Saudi Arabia dhidi ya watoto wadogo nchini Yemen.
Kwa upande wao, harakati za Answarullah ya Yemen na Hizbullah ya Lebanon nazo zimetoa taarifa tofauti kulaani mauaji ya kinyama yaliyofanywa na Saudia dhidi ya watoto hao wa Yemen.

Leave a Comment