Wakimbizi wa Sudan Kusini walioko Uganda kurejea nyumbani kuanzia Januari 2019.


Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema kuwa, wakimbizi wa Sudan Kusini walioko nchini mwake wanapaswa kurejea nchini kwao ifikapo Januari mwakani.
Rais Museveni amesema hayo jana katika mazungumzo yake mjini Dar es Salaam na Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kueleza kuwa, serikali ya Kampala ina matumaini kwamba, wakimbizi wapatao milioni moja wa Sudan Kusini wataanza kurejea kwao mwanzoni mwa mwaka ujao.
Rais wa Uganda ambaye jana alifanya ziara ya siku moja nchini Tanzania amesema kuwa, ana matumaini baada ya pande hasimu nchini Sudan Kusini kutiliana saini ya kuhitimisha mapigano na kugawana madaraka, wakimbizi wa nchi hiyo walioko Uganda watarejea nchini kwao.
Ameongeza kuwa, Uganda itaanza kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Sudan Kusini wanaoishi nchini humo kuanzia mwezi Januari mwaka 2019.
Wakati huo huo, Tanzania imethibitisha kuwa wakimbizi kutoka Burundi ambao wanaishi nchini humo wameanza kurejea nyumbani kwa hiari. Rais John Pombe Magufuli amesema, hii inatokana na hali ya amani kuanza kurejea katika nchi yao.
Katika mazungumzo yao jijini Dar es Salaam, mbali na masuala hayo ya kikanda, viongozi hao wawili walijadiliana kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga Tanzania, na kuwataka maafisa wa nchi hizo mbili kuharakisha mradi huo.
Uganda na Tanzania zimekubaliana pia kujenga reli ya kati itakayounganisha nchi hizo mbili kutokea Mwanza lakini pia kupambana na biashara ya magendo ya sukari inayotishia kuharibu soka la mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Leave a Comment