Tendai Biti Aachiliwa Huru Kwa Dhamana Nchini Zimbabwe.


Tendai Biti mmoja wa viongozi wa upinzani nchini Zimbabwe ambaye jana alipandishwa kizimbani katika mahakama mjini Harare ameachiliwa huuru kwa dhamana.
Tendai Biti ambaye alikataliwa ombi lake na serikali ya Zambia la kupatiwa hifadhi ya kisiasa alirejeshwa Zimbabwe kwa amri ya mahakama na sasa anakabiliwa na mashtaka ya kuchochea ghasia baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa Julai 30 mwezi uliopita.
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amesema kuwa, mwanasiasa huyo wa upinzani ameachiliwa huru kwa dhamana na mahakama baada ya yeye kuingilia kati.
Tendai Biti ni mwanasiasa wenye ushawishi mkubwa nchini Zimbabwe na ni Waziri wa zamani wa Fedha katika serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa na Rais wa zamani, Robert Mugabe na aliyekuwa Waziri Mkuu hayati Morgan Tsvangirai.
Vyombo vya usalama vya nchi hiyo vinatuhumiwa kwamba, vimekuwa vikitumia nguvu kupita kiasi kuwatawanya waandamanaji wanaolalamikia na kupinga matokeo ya uchaguzi uliopita.
Watu sita wameripotiwa kuuawa hadi sasa katika vurugu baina ya vyombo vya usalama na waandamanaji zilizozuka Agosti Mosi mwaka huu.
Uchaguzi wa kwanza wa Rais baada ya miaka 37 ya utawala wa Robert Mugabe ulifanyika nchini Zimbabwe tarehe 30 Julai. Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe Rais Emmerson Mnangagwa alishinda kwa asilimia 50.8 ya kura akifuatiwa na mgombea wa chama cha MDC Nelson Chamisa aliyepata asilimia 44.3 ya kura zote.

Leave a Comment