Chama tawala Sudan chamuunga mkono al Bashir kugombea mwaka 2020.


Chama tawala nchini Sudan kimemchagua Rais Omar al Bashir kugombea kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2020. Uamuzi huo umechukuliwa licha ya kwamba katiba ya Sudan inaruhu Rais kuwa madarakani kwa mihula miwili ya miaka mitano mitano.
Baraza la Ushauri la chama tawala cha Kongresi ya Taifa nchini Sudan kimemtangaza Omar al Bashir kuwa mgombea wake katika mkutano uliofanyika Khartoum mji mkuu wa nchi hiyo. Kiongozi huyo mkongwe amekuwa madarakani tangu baada ya mapinduzi ya jeshi ya mwaka 1989.
Kabashor Koko Mkuu wa Baraza la Ushauri la chama tawala nchini Sudan amesema kuwa uamuzi wa kumchagua Omar Hassan al Bashir ambaye alishinda chaguzi za mwaka 2010 na 2015 umechukuliwa na chama hicho katika ngazi zote. Amesema wameamua kuchukua hatua zote za lazima kuhakikisha kuwa al Bashir anagombea katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Itakumbukuwa kuwa katiba ya Sudan na hati zote za chama tawala cha Kongresi ya Taifa zinaruhusu mihula miwili tu ya urais na vipengee hivyo vyote vitapasa kufanyiwa marekebisho iwapo al Bashir atagombea tena kiti cha urais.

Leave a Comment