Rais wa Sudan Kusini awapa msamaha Machar na waasi wengine.


Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ametoa msamaha kwa waasi waliohusika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo akiwemo makamu wake wa zamani, Riek Machar.
Kufuatia msamaha huo, makundi ya kutetea haki za binadamu yamesema kuwa serikali ya nchi hiyo changa zaidi barani Afrika inapasa pia kuwaachia huru wapinzani.
Tangazo la msamaha huo limesomwa siku tatu baada ya Rais Kiir wa Sudan Kusini, kiongozi wa harakati ya ya waasi ya SPLM-IO Riek Machar na wakuu wa makundi mengine kusaini makubaliano ya kusitisha vita na kugawana madaraka huko Khartoum mji mkuu wa Sudan.
Mvutano wa kisiasa baina ya Kiir na Machar mwaka 2013 ulipelekea kuibuka vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilivyouwa makumi ya maelfu ya watu na kuilazimisha theluthi moja ya jamii ya nchi hiyo kukimbia makazi yao.
Wakati huo huo shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) leo limetoa wito wa kuachiwa huru wakosoaji kadhaa wa serikali ya Juba waliofungwa jela na idara za intelijinsia akiwemo Peter Biar Ajak mchumi mtajika ambaye amekuwa akizikosoa pande zote katika vita vya ndani huko Sudan Kusini.

Leave a Comment