King Majuto Kuzikwa Tanga.


Mwili wa nyota wa maigizo na vichekesho nchini, Amri Athuman (70) maarufu kwa jina la King Majuto unatarajiwa kuzikwa Tanga kesho.
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba amesema, mwili wa mzee Majuto utasafirishwa leo jioni kuupeleka mkoani humo.
King Majuto aliaga dunia jana saa moja na nusu usiku kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
“Jana (juzi) mimi nilikuja kumuona, wakasema sukari ilishuka sana, sukari imeshuka sana, sana, sana, sasa hata mimi nilivyokuwa namuona na hali yake kiukweli ilinitia hofu mno, alikuwa ni mtu ambaye amezidiwa sana…”amesema Mwakifamba.
Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kutokana na kifo cha msanii huyo mkongwe.
Rais Magufuli amemuagiza Waziri Mwakyembe afikishe salamu zake za pole kwa familia ya marehemu, wasanii wote nchini, wadau wa sanaa, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na kifo cha King Majuto.

Leave a Comment