Bunge la Libya lataka balozi wa Italia afukuzwe nchini humo.


Bunge la Libya limemtuhumu balozi wa Italia mjini Tripoli kuwa anaingila masuala ya ndani ya nchi hiyo na kutaka afukuzwe mara moja.

Mtandao wa habari wa al Wasat wa nchini Libya umetangaza usiku ya kuamkia leo kuwa, kamati ya masuala ya kigeni na ushirikiano wa kimataifa ya bunge la Libya imelaani matamshi ya balozi wa Italia mjini Tripoli, Giuseppe Perrone, aliyetaka kuakhirishwa uchaguzi wa Libya na kusema kuwa, matamshi hayo ni kinyume na protokali za kidiplomasia.
Kamati hiyo imesema kuwa matamshi hayo ni kuingilia waziwazi masuala ya ndani ya Libya na ni kukanyaga haki ya kitaifa ya kujiamulia yenyewe mambo yake nchi hiyo, hivyo imeitaka wizara ya mambo ya nje ya Libya imfukuze mara moja balozi huyo.
Siku chache zilizopita, balozi wa Italia mjini Tripoli alisema katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni moja kuwa yeye anapinga kufanyika uchaguzi huko Libya.
Balozi huyo aliituhumu baadhi ya mirengo ya Libya kuwa inashinikiza kufanyika haraka uchaguzi huo na kudai kuwa mirengo hiyo inataka kuhodhi madaraka.
Libya ilikuwa koloni la Italia kwa muda wa miaka 30 katika karne ya 20. Inasemekana kuwa Italia na Ufaransa zinafanya njama za kuwa na nafasi zaidi nchini Libya na hivi sasa kuna mvutano mkubwa baina ya madola hayo ya kikoloni ya Ulaya kuhusu nani ataweza kupora utajiri mkubwa zaidi wa mafuta wa Libya.

Leave a Comment