Wafugaji 11 wa Kifulani wauawa katika machafuko mapya Mali.


Raia 11 wa kabila la Fulani wametekwa nyara na kuuawa katika machafuko mapya ya kikabila kuikumba nchi ya Mali. Mauaji hayo yamefanyika katika mji wa Mopti katikati mwa Mali.
Abdoul Aziz Diallo kiongozi wa jumuiya ya kabila la Fulani la Tabital Pulaaku amesema kuwa wanamgambo wa jamii ya Dogon Jumanne wiki hii waliawaua raia 11 wa Fulani wakati walipokuwa wakielekea katika soko la Sofara. Wanamgambo hao walifika sokoni hapo kwa kutumia pikipiki.
Mivutano na machafuko kati ya wafugaji wa kabila la Fulani na wakulima wa makabila ya Bambara na Dogon vimepamba moto katikati mwa Mali. Machafuko hayo yalishtadi baada ya kuzagaa tuhuma kwamba watu wa jamii ya kabila la Fulani wanashirikiana na wanamgambo wa kitakfiri wenye misimamo mikali.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa raia zaidi ya 300 wa Mali wameuawa katika machafuko ya kikabila tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2018.

Leave a Comment