Vikosi vya Yemen vyatungua ndege ya kivita ya Saudia.


Kikosi cha Anga cha Jeshi la Yemen kimefanikiwa kudungua ndege ya kivita ya Saudi Arabia kusini mashariki mwa ardhi ya Saudia.
Wizara ya Ulinzi ya Yemen imesema vikosi vya Yemen vilitungua ndege hiyo ya Saudia jana Alkhamisi katika eneo la Asir, kusini mashariki mwa Saudi Arabia, ikitokea mkoa wa Sa’ada, kaskazini mwa Yemen.
Haya yanajiri chini ya masaa 48 baada ya Jeshi la Yemen, likishirikiana na wapiganaji wa Kamati za Wananchi, kuvurumisha kombora lililotengenezwa nchini humo na kulenga kambi ya mamluki wa Saudi Arabia ambao ni watiifu kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Abd Rabbuh Mansur Hadi katika mji wa al Hudaydah katika pwani ya magharibi mwa nchi hiyo.
Oparesheni hiyo ya ulipizaji kisasi ilitekelezwa masaa machache baada ya ndege za kivita za Saudia kudondosha mabomu katika nyumba za makazi katika pembe tofauti za Yemen ambapo raia kadhaa wasio na hatia waliuawa na wengine kujeruhiwa.
Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi makali ya kikatili dhidi ya wananchi Waislamu wa Yemen mwezi Machi 2015 kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Imarati na kwa kutumia silaha zinazopewa na nchi za Magharibi.
Hadi sasa watu karibu 15,000, wengi wakiwa ni watoto na wanawake wameshauawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa huko Yemen na mamilioni wakiachwa bila makao.
Aidha hujuma hiyo ya Saudia, ambayo inapata himaya ya utawala haramu wa Israel, Uingereza na Marekani, imepelekea Yemen kukumbwa pia na janga la umaskini, ukame na miripuko ya magonjwa mbalimbali hatari ya kuambukiza kama vile kipindupindu.

Leave a Comment