Mashambulizi ya anga ya Marekani nchini Syria yaua 30 mjini Bukamal.


Kwa akali raia 30 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani katika mji wa Bukamal, mkoa wa Dayr al-Zawr mashariki mwa Syria.
Shirika rasmi la habari la Syria SANA limeripoti kuwa, muungano huo wa Marekani unaodai kuwa unapambana na magaidi wa Daesh (ISIS) nchini Syria umefanya hujuma hiyo leo Ijumaa viungani mwa mji huo muhimu na kulenga makazi ya raia, ambapo wanawake na watoto wadogo ni miongoni mwa wahanga wa ukatili huo.

Duru za habari zimearifu kuwa, yumkini idadi ya wahanga wa mashambulizi hayo ya ndege za kivita za Marekani na waitifaki wake ikaongezeka, kutokana na majeraha mabaya waliyoyapata wakazi wa mji huo.
Novemba mwaka jana, Jeshi la Syria, wapiganaji wa Hizbullah na washirika wao walifanikiwa kuukomboa mji huo wa Bukamal ulioko kwenye ufukwe wa Mto Furati na mpakani na Iraq, kutoka kwenye makucha ya kundi la Kiwahabi la Daesh.
Serikali ya Damascus imekuwa ikisisitiza kuwa, lengo la Marekani kuingia katika nchi hiyo ya Kiarabu bila ridhaa ya serikali ni kuyaunga mkono na kuyashajiisha magenge ya kigaidi.
Mgogoro wa Syria uliibuka mwaka 2011 baada ya magaidi wanaoungwa mkono na Saudi Arabia, Utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani na waitifaki wao kuanzisha mashambulio kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Bashar al-Assad, njama zilizoshindwa kuzaa matunda kutokana na kusimama kidete jeshi la Syria na waitifaki wake.

Leave a Comment