Baraza la Usalama la UN laiwekea vikwazo Sudan Kusini.


Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeiwekea vikwazo vya silaha nchi ya Sudan Kusini, karibu miaka mitano sasa baada ya nchi hiyo kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Azimio la vikwazo dhidi ya Sudan Kusini limepasishwa na nchi 9 wanachama wa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huku nchi kama Russia, China, Ethiopia, Bolivia, Equatorial Guinea na Kazakhstan zikijizuia kuupiga kura muswada uliowasilishwa na Marekani wakati huu ambapo kunafanyika jitihada za kikanda za kukomesha mgogoro wa ndani wa Sudan Kusini.
Balozi wa Ethiopia katika Umoja wa Mataifa, Tekeda Alemu ameliambia Baraza la Usalama kabla ya kupigiwa kura muswada huo kwamba, kuweka vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan Kusini yumkini kukatatiza mchakato wa kurejesha amani na kwamba Umoja wa Afrika (AU) na jumuiya ya kikanda ya IGAD zinaamini kwamba, huu si wakati mwafaka wa kuchukuliwa hatua kama hiyo.
Vilevile balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Ma Zhaoxu amesema Baraza la Usalama lilipaswa kusikiliza sauti ya viongozi wa Afrika katika kadhia hiyo.
Baada ya kupasishwa muswada huo balozi wa Sudan Kusini katika Umoja wa Mataifa, Akuei Bona Malwal ameliambia Baraza la Usalama kwamba azimio hilo litavuruga amani na kwamba ni pigo kwa taasisi zinazofanya jitihada za kurejesha amani Sudan Kusini.
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.

Leave a Comment