Upinzani Sudan Kusini wapinga kurefushwa muda wa uongozi wa Kiir.


Saa chache baada ya Bunge la Sudan Kusini kupiga kura na kuunga mkono kurefushwa muda wa Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kubakia madarakani hadi mwaka 2021, upinzani unaoongozwa na Riek Machar umejitokeza na kukosoa vikali hatua hiyo.
Mabior Garang de Mabior, msemaji wa kundi la waasi la SPLM- IO ameitaja hatua hiyo ya bunge kuwa kinyume cha sheria na kusisitiza kuwa itaufanya mchakato wa kupatikana amani nchi humo kuwa mgumu zaidi.
Amesema, “Kitendo hicho kinaonesha namna utawala wa Kiir unavyoyachezea shere mazungumzo ya amani. Jamii ya kimataifa haipaswi kuitambua hatua hiyo na inapaswa kuutambua utawala wa sasa kama utawala wenye kiburi.”
Hata hivyo serikali imetoa hoja kwamba hatua ya kuongeza muda kwa viongozi wa mpito nchini humo kwa miaka mitatu ni muhimu ili kuepuka ombwe la uongozi. Iwapo Rais Kiir ataidhinisha sheria hiyo, uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike nchini humo mwaka huu utasogezwa mbele hadi mwaka 2021.
Haya yanajiri siku chache baada ya waasi hao ambao kwa sasa ndio wapinzani nchini humo kukataa pendekezo la kumrejesha kiongozi wao Riek Machar kama makamu wa rais wa Salva Kiir.
Hii ni katika hali ambayo, Lam Paul Gabriel, msemaji wa waasi nchini humo alisema siku chache zilizopita kwamba askari wapatao 200 wa serikali ya Sudan Kusini wameshambulia kituo kimoja cha waasi kilichoko katika mkoa wa Mto Yei, sanjari na kukosoa safari ya mkuu wa majeshi ya Sudan Kusini huko China kwa madai kuwa safari hiyo imefanyika kwa ajili ya kwenda kununua silaha mpya, jambo ambalo amelitaja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa mapatano ya usitishaji vita.

Ijumaa iliyopita viongozi hao wa Sudan Kusini walikubaliana kuondoa askari wao katika maeneo yote ya mijini na ya makazi ya raia, siku mbili baada ya kusaini makubaliano ya amani huko Khartoum nchini Sudan.

Leave a Comment