Uhusiano wa Kistratijia wa Iran na Russia hauathiriwi na wengine.


Ali Akbar Velayati, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa, akizungumza Alhamisi punde baada ya mazungumzo yake na Rais Putin amesema: “Mkutano huu ulikuwa mzuri, wa wazi na wa kirafiki na tumezungumza kuhusu masuala yanayohusu pande mbili.”
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia ni nchi mbili zenye misimamo na sera huru na za kujitegemea na ni nchi muhimu katika mlingano wa kieneo. Russia na Iran zinashuhudia kiwango kipya cha uhusiano wa pande mbili katika masuala mbali mbali. Ushirikiano chanya na athirifu wa Iran pamoja na Russia katika mgogoro wa Syria ni jambo ambalo limebadilisha mlingano wa kisiasa na kijeshi katika nchi hiyo kwa maslahi ya serikali halali ya Rais Bashar al Assad.
Leo, kutokana na mtazamo chanya wa viongozi wa Iran na Russia kuhusu kiwango cha ushirikiano wa nchi mbili tunashuhudia kuzidi kuimarika zaidi uhusiano huo.
Kiwango cha sasa cha ushirikiano wa Iran na Russia kimejengeka katika msingi wa ‘washirika wenye kuaminiana’ na hii ni ishara nzuri katika mustakabali wa Tehran na Moscow.
Kuhusiana na nukta hiyo, Levan Dzhagaryan balozi wa Russia nchini Iran siku ya Jumanne alisema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mshirika mwenye thamani kubwa kwa Russia na ina nafasi muhimu katika sera za kigeni za Moscow.”
Ushirikiano na uhusiano mzuri wa Iran na Russia ni ishara ya mitazamo sawa ya viongozi wa nchi hizi mbili katika masuala ya kieneo na kimataifa.
Kwa kuzingatia mitazamo hiyo, Iran na Russia zimetumia njia za kimantiki na zenye busara katika kuathiri matukio ya Syria. Ni kutokana na muelekeo huo ndio mlingano wa kijeshi na kisiasa nchini Syria ukabadilika kwa maslahi ya serikali halali ya nchi hiyo na mrengo wa muqawama au mapambano. Mafanikio hayo yanahitaji mazungumzo na mawasiliano ya mara kwa mara ya viongozi wa ngazi za juu wa Iran na Russia na ni katika fremu hiyo ndio ukafanyika mkutano baina ya Mshauri wa Kiongozi Muadhamu katika masuala ya Kimataifa na Rais wa Russia mjini Moscow.
Akizungumza kuhusu safari ya Dkt. Velayati mjini Moscow, Hussein Amir Abdulahian msaidizi maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, katika masuala ya kimataifa amesema: “Mazungumzo ya wazi ya wakuu wa Iran na Russia katika kiwango cha juu na kubadilishana mitazamo kunaweza kukurubisha zaidi mitazamo ya viongozi wa nchi mbili na hivyo pande mbili ziweze kutafuta njia muafaka za kuimarisha uthabiti na usalama katika eneo na kukabiliana na sera mbovu za Marekani na waitifaki wake.”
Iran na Russia mbali na kushirikiana katika masuala ya kieneo na kimataifa pia zina uhusiano mzuri wa pande mbili.
Ushirikiano wa nchi mbili katika sekta ya nyuklia ambao umepelekea kujengwa kituo cha nyuklia cha Bushehr pembizoni mwa Ghuba ya Uajemi ni nembo ya ushirikiano wa Moscow na Tehran. Leo viongozi wa Russia na Iran wanazingatia kwa kina uhusiano mzuri wa pande mbili katika masuala mbali mbali kama vile mafuta na gesi.
Kwa kuzingatia matukio ya baada ya Marekani kuchukua uamuzi wa upande mmoja na ulio kinyume cha sheria wa kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama ‘Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA, Russia kama mshirika mwenye kuaminika wa Iran ina nafasi athirifu katika uhusiano wa kiuchumi wa nchi mbili.

Leave a Comment