Rais wa Eritrea kuitembelea Ethiopia kesho Jumamosi ya Tarehe 14 Julai 2018.


Rais wa Eritrea Isaias Afwerki anatazamiwa kuelekea nchini Ethiopia kesho Jumamosi, siku chache baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Ethiopia mjini Asmara.

Waziri wa Habari wa Eritrea, Yemane Meskel amethibitisha kuhusu safari hiyo leo Ijumaa na kuandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: Ziara hii itaongeza chachu katika mchakato wa amani ya kudumu na ushirikiano endelevu wa pande mbili.
Jumatatu iliyopita, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alifika katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara, na kukutana na rais wa nchi hiyo Isaias Afwerki ambapo pande mbili zilitiliana saini mapatanao ya kumaliza ‘ hali ya vita’ ambayo imekuwepo baina ya nchi hizo mbili kwa miongo miwili sasa.
Baada ya kufanya ziara hiyo mjini Asmara, Abiy Ahmed alisema serikali yake iko tayari kutekeleza mapatano yaliyofikiwa ili kuwawezesha wananchi wa Ethiopia na Eritrea kupata fursa bora zaidi.
Eritrea ilijitenga na Ethiopia mwaka 1993 na kisha kukata uhusiano wa pande mbili na hivyo kupelekea Ethiopia ikose njia ya bahari.
Mwaka 1998 kuliibuka vita vikali na mzozo wa mpakani baina ya nchi hizo ambao ulipelekea watu zaidi ya 80,000 kupoteza maisha na malaki kuachwa bila makao.
Mwaka 2000 Umoja wa Mataifa ulizipatanisha pande mbili hizo na kusema eneo la mpakani lililokuwa likizozaniwa ni milki ya Eritrea lakini mapatano hayo ya amani hayakutekelezwa.
Hatimaye mwezi jana Waziri Mkuu wa Ethiopia aliwashangaza wengi alipokubali mapatano hayo ya amani.

Leave a Comment