Ummy aagiza dereva gari la wagonjwa asimamishwe.


Simiyu. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tarime, Elias Ntiruhungwa kumsimamisha kazi dereva wa gari la kubeba wagonjwa la halimashauri hiyo aliyekamatwa akiwa amepakia kilo 800 za mirungi.
Kauli hiyo imetolewa Alhamisi ya Julai 12,2018 katika uzinduzi wa mradi wa Tuwatumikie katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.
Amesema mbali na dereva huyo, maofisa waliokuwa wamepanda gari hilo nao wasimamishwe kazi.
‘’Nimesikitishwa na taarifa za kukamatwa kwa gari la wagonjwa likiwa na mirungi,inasikitisha maana magari yanabadilishwa matumizi huku wagonjwa wakipata shida na wengine hata kufarika dunia,’’ amesema.
Amewataka waganga wakuu wa Wilaya na Mikoa kusimamia matumizi sahihi ya magari hayo ili wagonjwa wawe wanafika kwa haraka katika vituo vya afya kwa ajili ya matibabu.
Amesisitiza kuwa hataki kuona magari ya wagonjwa yanafanya shughuli nyingine na kuagiza kuwa yanapaswa kuwa katika vituo vya afya yalivyopangiwa.
Chanzo:MWANANCHI 12/07/2018

Leave a Comment