Vikosi vya Yemen vyazima mashambulizi ya Saudia al-Hudaydah.


Jeshi la Yemen likishirikiana na vikosi vya kujitolewa vya wananchi limefanikiwa kuzima mashambulizi ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, dhidi ya bandari ya al-Hudaydah ambayo ndilo lango kuu la kuingizia misaada ya kibinadamu kwa raia wanaoendelea kuua ovyo wa Yemen.
Dayfallah al-Shami, afisa wa ngazi za juu wa harakati ya Ansarullah ya Yemen ameiambia kanali ya televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon kuwa, vikosi hivyo vya Yemen vimefanikiwa kuzuia wanajeshi wa Saudi na Umoja wa Falme za Kiarabu kukaribia bandari hiyo ya kistratajia.
Muungano vamizi unaoongozwa na Saudia Arabia dhidi ya Yemen ulianzisha mashambulizi makali hapo jana kwa shabaha ya kutwaa bandari ya al-Hudaydah.
Wakati huo huo, shirika la habari la serikali ya Imarati WAM limetangaza habari ya kuuawa wanajeshi wanne wa UAE katika uvamizi huo wa jana Jumatano.
Muungano wa kijeshi wa Saudia ulizindua mashambulizi makali yenye lengo la kutwaa bandari ya al-Hudaydah, licha ya Umoja wa Mataifa kuonya kuwa, hujuma dhidi ya bandari hiyo yumkini ikasababisha vifo vya watu zaidi ya laki 2 na 50 elfu.
Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi makali ya kikatili dhidi ya wananchi Waislamu wa Yemen mwezi Machi 2015 kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Imarati na kwa kutumia silaha zinazopewa na nchi za Magharibi.
Hadi hivi watu karibu 15,000, wengi wakiwa ni watoto na wanawake wameshauawa na makumi ya maelefu ya wengine kujeruhiwa huko Yemen na mamilioni wakiachwa bila makao. Aidha hujuma hiyo ya Saudia, ambayo inapata himaya ya utawala haramu wa Israel, Uingereza na Marekani, imepelekea Yemen kukumbwa pia na janga la umaskini, ukame na miripuko ya magonjwa mbalimbali hatari ya kuambukiza kama vile kipindupindu.

Leave a Comment