Saudia yaanzisha ‘rasmi’ mashambulizi dhidi ya bandari ya al-Hudaydah, Yemen.


Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umeanzisha ‘rasmi’ mashambulizi makali dhidi ya bandari ya kistratajia ya al-Hudaydah, huku ukilipa sikio la kufa tahadhari ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu yaliyoonya juu ya matokea mabaya ya hatua hiyo ya kijeshi.
Kanali ya televisheni ya Al Arabiya inayomilikiwa na Riyadh imetangaza mapema leo Jumatano kuhusu kuanza mashambulizi ya anga ya Saudia dhidi ya bandari hiyo iliyoko katika Bahari Nyekundu, sambamba na kuanza hujuma ya ardhini ya vikosi vya Umoja wa Falme za Kiarabu.
Imarati ilikuwa imewapa muhula wa hadi jana Jumanne wanaharakati wa Ansarullah wawe wameondoka katika bandari hiyo.
Haya yanajiri siku chache baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kusema kuwa, mjumbe wake katika masuala ya Yemen, Martin Griffiths anashauriana na nchi za Saudia na Imarati na kwamba kuna matumaini mazungumzo hayo yatazuia kutokea maafa ya binadamu katika bandari ya al-Hudaydah.
UN tayari imeonya kuwa, mashambulizi dhidi ya bandari hiyo yumkini yakasababisha vifo vya watu zaidi ya laki 2 na 50 elfu.
Huku hayo yakiarifiwa, Naibu Mkuu wa Idara ya Habari ya harakati ya Ansarullah ya Yemen, Abdul Quddus al Shahari amekataa pendekezo la kukabidhi bandari hiyo muhimu kwa Saudia na washirika wake na kusema jeshi la Yemen na wapiganaji wa kujitolea hawatakabidhi bandari hiyo ambayo ndilo lango pekee la kuingizia bidhaa za chakula kwa Wayemen.

Leave a Comment