Assad: Vikosi vya Israel na Uturuki vilivyoko Syria ni vamizi.


Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema vikosi vya utawala wa Kizayuni wa Israel, Uturuki, Marekani na Ufaransa vilivyoko nchi humo ni vikosi vamizi.
Assad aliyasema hayo jana Jumatano katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Alam na kuongeza kuwa, msimamo wa Syria ni kuunga mkono harakati za muqawama zinazopambana dhidi ya magaidi na vikosi vamizi, pasina kujali utaifa wao.
Amebainisha kuwa, hakuna vituo vya kijeshi vya Iran nchini humo, lakini Damascus haitasita kuruhusu uwepo wa vituo hivyo iwapo italazimu. Rais wa Syria amesisitiza kuwa, waungaji mkono wa magenge ya kigaidi nchini Syria wamekuwa wakitoa matamshi ya uwongo na yasiyo na msingi ili kuyashajiisha na kuyapa moyo makundi hayo ya kigaidi yanayoelekea kusambaratika kikamilifu.
Wiki iliyopita katika mahojiano na gazeti la Daily Mail, Rais Assad alisema madola ya Magharibi hayawezi kuiainishia nchi hiyo mustakbali wake na kusisitiza kuwa, wanajeshi wa Uingereza na Marekani walioko nchini humo ni wavamizi.
Marekani, Ufaransa na Uingereza zimetuma wanajeshi wao vamizi kinyume cha sheria nchini Syria kwa madai ya eti kupambana na ugaidi.
Syria ilitumbukizwa kwenye mgogoro mkubwa mwaka 2011 baada ya nchi za Magharibi kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za eneo hasa Saudi Arabia, kumimina magaidi kutoka kila kona ya dunia ndani ya ardhi ya Syria, na kuwapa silaha na mafunzo ya kijeshi ili wavuruge amani na uthabiti katika nchi hiyo ya Kiarabu, na kuandaa uwanja wa kumng’oa madarakani rais halali wa nchi hiyo.

Leave a Comment