Riek Machar akubali kukutana ana kwa ana na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini.


Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar amekubali kukutana ana kwa ana na Rais Salva Kiir wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika, wiki ijayo nchini Ethiopia.
Msemaji wa Machar amesema katika taarifa iliyotolewa jana Jumatano kwamba, kiongozi huyo wa waasi wa Sudan Kusini ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha nyumbani nchini Afrika Kusini amekubali mwaliko wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ambaye amemtaka wakutane katika kikao cha moja kwa moja na Rais Kiir, katika mji mkuu Addis Ababa, mnano Juni 20.
Taarifa ya msemaji wa Riek Machar imesema mazungumzo hayo yataongozwa na Jumuiya ya Kiserikali ya Maendeleo Mashariki mwa Afrika IGAD. Hata hivyo IGAD haijatoa taarifa kuhusu kadhia hiyo kufikia sasa.
Hii ni katika hali ambayo mapema mwezi huu, jumuiya hiyo ya kieneo ilionekana kusalimu amri katika jitihada za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini Sudan Kusini, baada ya kusema kuwa, “Hata umlete Malaika Jibril awe mpatanishi, hilo halitakuwa na tija yoyote. Jitihada za upatanishi zitazaa matunda pale tu Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar watakapoamua kukutana ana kwa ana, na wakubaliane kuhusu njia za kufanikisha mchakato wa amani ya kudumu katika taifa lao.”
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.

Leave a Comment