Qatar yamteua balozi mpya maalumu kuhudumu Iran.


Sheikh Tamim bin Hamad, Amiri wa Qatar, amemteua Mohammed bin Hamad Al Hajri kuwa balozi mpya maalumu wa nchi hiyo katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Cheo cha balozi maalumu mwenye mamlaka kamili (extraordinary and plenipotentiary) ni cheo cha juu zaidi cha kidiplomasia ambacho balozi anaweza kupewa na hivyo kumfanya atambulike pia kama mjumbe maalumu.
Baada ya Oman, Qatar ndio nchi yenye uhusiano mzuri zaidi na Iran miongoni mwa nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Kinyume na Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar imekuwa ikijiepusha kuwa na msunguano katika uhusiano wake na Iran na badala yake imekuwa ikijitahidi kuwa na uhusiano mzuri na Jamhuri ya Kiislamu.
Katika kuwepo uhusiano huo mzuri, nchi mbili zimejitahidi kutoathiriwa na migogoro inayojiri katika eneo lenye misuguano mikali la Mashariki ya Kati. Mbali na hayo kuna nukta kadhaa ambazo zimepelekea Qatar na Iran kutaka kuwa na uhusiano mzuri kama vile mpaka wa pamoja wa baharini na kuwa na eneo la pamoja na uchimbaji gesi baharini. Uhsiano wa nchi hizi mbili pia umeathiriwa na sera za Saudi Arabia katika eneo.
Kuna hali ya kutoaminiana katika uhusiano wa Iran na Saudia Arabia, ambayo pamoja na Uturuki zinahesabiwa kuwa washindani wakuu wa Iran katika eneo.

Leave a Comment