Kabila wa DRC afuata nyayo za Nkurunziza, asema hatagombea muhula wa tatu wa urais.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo hatagombea muhula wa tatu wa urais katika uchaguzi unaotazamiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Bruno Tshibala amesema uchaguzi wa Disemba mwaka huu utafanyika bila ushiriki wa Rais Joseph Kabila ambaye amefanya hivyo kutokana na moyo wa kuheshimu katiba ya nchi.
Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Pierre Nkrunziza wa Burundi kutoa tangazao la kushtukiza kwamba hatawania urais katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020.
Waziri Mkuu wa Kongo DR amesema uchaguzi huo utafanyika Disemba 23 kama ilivyopangwa, na Rais Kabila atahudhuria mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika mjini Luanda wiki ijayo, ambapo atawahakikishia wakuu hao wa AU azma ya DRC kuheshimu katiba na kutekeleza ahadi yake ya uchaguzi.
Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi uliopita, chama tawala cha People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD) kilibandika mabango yenye picha za kiongozi wao huyo kuanzia mijini hadi vijijini, mbali na kutengeneza fulana zenye picha za Kabila na kuzigawa kwa watu katika kila kona ya nchi, na haswa ngome za kisiasa za rais huyo, hatua mbayo viongozi wa upinzani nchini humo walisema ni kumuandalia Kabila mazingira ya kuwania muhula wa tatu kinyume cha sheria.
Ieleweke kuwa, Joseph Kabila alikataa kuachia madaraka baada ya kumalizika muhula wake wa utawala kikatiba mwaka 2016, na mpaka sasa binafsi hajajitokeza hadharani kusema iwapo atagombea au ataachia ngazi baada ya uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika Disemba 23 mwaka huu.

Leave a Comment