Watu wawili wauawa kwa kudungwa visu msikitini nchini Afrika Kusini.


Kwa akali watu wawili wamethibitishwa kuuawa kwa kudungwa visu wakiwa msikitini, baada ya mtu mmoja kuvamia eneo hilo la ibada nchini Afrika Kusini.
Noliyoso Rwexana, msemaji wa polisi katika mkoa wa Western Cape amesema tukio hilo limefanyika leo alfajiri katika mji wa Malmesbury, ulioko kusini mwa mkoa huo.
Amesema watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika shambulizi hilo na kwamba gaidi aliyehusika na hujuma hiyo pia ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Haya yanajiri mwezi mmoja bada ya polisi nchini Afrika Kusini kugundua kifurushi cha mada za milipuko katika msikiti wa Imam Hussein AS katika mji mdogo wa Verulam nje ya Durban; msikiti ambao juma moja kabla ya hapo ulikuwa umevamiwa na magaidi.
Mei 10, watu wanaosadikiwa kuwa magaidi wakufurishaji waliuvamia msikiti huo wa Imam Hussein AS karibu na mji wa Durban Afrika Kusini na kumuua shahidi Imamu wake kwa kumkata kichwa na kuwajeruhi waumini wengine kadhaa.
Magaidi hao waliokuwa na silaha mbali na kumuua Imamu wa msikiti waliwashambulia waumini kwa kuwadunga visu na kuwajeruhi kadhaa miongoni mwao.

Leave a Comment