Wanawake 500 kujadili fursa leo.


Takribani wanawake 500 kutoka nchi 25 za Afrika, wanatarajiwa kukutana nchini leo, katika kongamano la kuwakutanisha pamoja wanawake (Africa Reconnect), kwa ajili ya kujadili fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo namna ya kujiinua kiuchumi kupitia mapinduzi ya viwanda.
Kongamano hilo litakalohudhuriwa na wanawake wa kada mbalimbali wakiwemo wake wa marais, watoa maamuzi na watunga sera, wanawake viongozi mbalimbali na wanasiasa linatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Washiriki wengine katika kongamano hilo ni kutoka sekta mbalimbali zikiwemo biashara, taasisi za fedha, madini, ujenzi, michezo, uwekezaji, wanawake wajasiriamali wa kada mbalimbali ikiwemo kada za chini, sekta binafsi, wizara mbalimbali, maofisa wa serikali, asasi za kijamii na wanataaluma mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo, Dar es Salaam jana, Mratibu wa African Reconnect nchini, Anjela Bondo, alisema kongamano hilo lilishaanza tangu Mei 14, mwaka huu kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kutoka vikundi 150 vya wanawake Tanzania na wanawake 50 kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Alisema kuanzia leo baada ya uzinduzi wa kongamano hilo lenye kaulimbiu ‘Kuwainua Wanawake wa Afrika katika Mapinduzi ya Viwanda’, lengo lake ni kutoa fursa kwa wanawake kujadili na kupitia fursa zilizopo katika kuwawezesha kimaendeleo ambapo kwa mwaka huu, limeangazia zaidi eneo la mapinduzi ya viwanda.
Alisema wakati Tanzania ikitekeleza maono yake ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025, kongamano hilo limejipanga kuhakikisha linawapatia ujuzi wanawake katika kutumia teknolojia na hivyo kuboresha viwango vya bidhaa zao.
Bondo alisema pamoja na fursa hizo, katika kongamano hilo kutawasilishwa mada mbalimbali. Watakaowasilisha mada hizo ni pamoja na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko kutoka Zanzibar Amina Salum Ali, Ofisa Mtendaji Mkuu kutoka kampuni ya Jambo Plastics, Rupa Suchacl na Mwanamuziki kutoka Afrika Kusini na Mjasiriamali, Yvonne Chakachaka.
Wengine ni Malkia kutoka Swaziland, Dk Sibonelo Mbikiza, Waziri wa Utalii mstaafu wa Zimbabwe, Anastacia Ndhlovu, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake Tanzania, Mary Rusimbi na Mkurugenzi wa TTB, Devotha Mdachi.

Kongamano la kwanza la Africa Reconnect lilifanyika Afrika Kusini mwaka 2013, la pili Limpopo Afrika Kusini mwaka 2015 na la tatu lilifanyika Abuja, Nigeria mwaka 2016. Kongamano linafadhiliwa na taasisi mbalimbali na baadhi yake ni TTB, Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN) wachapishaji wa magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo na SpotiLeo, Benki ya Azania, Vodacom na Coca-Cola.
Chanzo:HabariLeo 17/05/2018

Leave a Comment