Ummy ahimiza wanawake kutumia kilimo kujikwamua.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu amewataka wanawake wa Afrika wakiwemo Watanzania kutumia fursa ya ardhi kubwa iliyopo Afrika kujiendeleza kupitia kilimo.
Waziri huyo amebainisha kuwa kwa sasa kilimo ndiyo sekta iliyoajiri watu wengi hususani Afrika ambapo kwa Tanzania asilimia kubwa ya wanawake Tanzania wanajishughulisha au kujihusisha na kilimo.
Akifungua kongamano lililokutanisha wanawake wa Afrika pamoja (Afrika Reconnect), kwa niaba ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri huyo alisema pia kwa mujibu wa takwimu zilizopo takribani asilimia 65 ya ardhi duniani kote ambayo haijatumika iko Afrika.
“Ili tuweze kuufikia uchumi au mapinduzi ya viwanda, wanawake inabidi tuinuke tuitumie ardhi hii katika kilimo, tuzalishe kwa wingi bidhaa bora, zitumike kwenye viwanda vyetu,” alisema. Alisema anaamini kuwa eneo ambalo wanawake watafanya vizuri na kujiinua kiuchumi kupitia viwanda ni eneo la Sekta ya Kilimo.
Alisema pamoja na kwamba eneo hilo ndiyo ajira kuu ya Waafrika wakiwemo Watanzania, lakini ndiyo eneo muhimu linalozalisha malighafi zinazotumika viwandani.
Alisema ili wanawake wa Afrika wawe sehemu ya mapinduzi ya viwanda, serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali wanahitaji kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja katika kuwajengea uwezo wanawake ili waweze kuendana na teknolojia za kisasa.
Akizungumzia kongamano hilo la Africa Reconnect alisema ni fursa kwa Watanzania hasa kutokana na kaulimbiu yake ya ‘Kuwainua Wanawake Kupitia Uchumi wa Viwanda’ kwani inaendana na maono ya Tanzania ya mwaka 2025 ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia viwanda.
Taasisi mbalimbali nchini zimefadhili kongamano hilo, baadhi yake ni TTB, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) wachapishaji wa magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo, Habari Leo Jumapili na SpotiLeo, Benki ya Azania Bank, Vodacom na Cocacola.
Chanzo:HabariLeo 18/05/2018

Leave a Comment