Hali ya taharuki yatanda Kongo DR na nchi jirani kufuatia kusambaa ugonjwa hatari wa Ebola.


Wasi wasi umetanda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi jirani na taifa hilo kutokana na kuripotiwa kusambaa ugonjwa hatari wa Ebola.
Kufuatia hali hiyo, nchi zinazoizunguka Kongo DR zimewataka raia wake kuchukua tahadhari kubwa sambamba na kuimarisha ukaguzi katika maeneo ya mipakani na kutangaza kuwapima viwango vya joto wageni wote wanaoingia katika nchi hizo hususan kwa wale wanaotumia usafiri wa ndege. Katika uwanja huo, Waziri wa Afya wa Kenya, Sicily Kariuki amesema kuwa, sasa wasafiri wote wanaofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na vituo vya mpakani vya Busia na Malaba watakuwa wakipimwa viwango vyao vya joto la mwili.
Mbali na Kenya serikali ya Tanzania kupitia Wizara yake ya Afya mbali na kuthibitisha kuzuka upya kwa ugonjwa huo, imetoa maelekezo muhimu kwa wananchi. Hivi karibuni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliwatoa hofu wananchi, ingawa hakuondoa uwezekano wa taifa hilo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa hatarini kukumbwa na ugonjwa huo. Alisema kuwa, pamoja na kwamba hadi hakuna mgonjwa aliyethibitika kukumbwa na ugonjwa huo, lakini hiyo haimanishi kwamba wananchi waendelee kubweteka wakati nchi jirani inahangaika. Kwa ajili hiyo, alisema serikali imeamua kuimarisha udhibiti na ukaguzi katika maeneo ya mipakani ili kujilinda na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa serikali ya Tanzania, operesheni hiyo imeelekezwa zaidi katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa maeneo ambayo yana muingiliano wa karibu na raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Jamhuri ya Kidemokrasia ya ilikumbwa kwa mara ya kwanza na ugonjwa huo mwaka 1976 Miladia wakati ambao taifa hilo lilikuwa likiitwa Zaire.
Aidha kuibuka tena maradhi hayo kunaifanya nchi hiyo kuwa imekumbwa mara tisa tangu ugonjwa huo ulipodhibitiwa mwaka 76.

Leave a Comment