Korea Kaskazini: Hatutofanya mazungumzo na Korea Kusini kabla ya kutatuliwa masuala muhimu.


Serikali ya Korea Kaskazini imesema kuwa, haitofanya mazungumzo na Korea Kusini kabla masuala muhimu hayajatatuliwa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Amani nchini Korea Kaskazini, Ri Sun Gun na kuongeza kuwa, maneva ya kijeshi ya pamoja ya Korea Kusini na Marekani ni ya uchochezi, na amelikosoa vikali pia bunge la nchi hiyo jirani.
Uwepo kijeshi wa Marekani katika Rasi ya Korea, kufanya maneva ya pamoja majeshi ya Marekani na Korea Kusini na kadhalika usimikaji wa ngao ya makombora ya Marekani aina ya THAAD ndani ya nchi hiyo jirani, ni miongoni mwa masuala ambayo Korea mbili zimekuwa zikihitilafiana.
Katika kulalamikia kuanza maneva ya majeshi ya anga ya Marekani na Korea Kusini, hivi karibuni Pyongyang ilivunja mazungumzo ya ujumbe wa ngazi ya juu wa kisiasa wa Korea Kusini ambayo yalikuwa yamepangwa kufanyika siku ya Jumatano katika ngazi ya mawaziri wa nchi mbili.
Kadhalika Pyongyang imetishia kwamba huwenda ikavunja ratiba ya mazungumzo kati ya Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini na Rais Donald Trump wa Marekani ambayo yamepangwa kufanyika mwezi ujao nchini Singapore kutokana na kuendelea maneva hayo ya kijeshi yanayofanyika katika Rasi ya Korea. Katika hatua nyingine ujumbe wa India umeingia nchini Korea Kaskazini baada ya kupita miongo miwili.
Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema kuwa, hivi karibuni na kwa mara ya kwanza mawaziri kadhaa wa nchi yake waliwasili mjini Pyongyang ambapo mbali na kukutana na viongozi wa ngazi ya juu wa taifa hilo, walitiliana saini mikataba kadhaa.
Mara ya mwisho kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa India kutembelea Korea Kaskazini ilikuwa mwaka 1998 baada ya Waziri wa Vyombo vya Habari wa nchi hiyo kufanya safari nchini humo.

Leave a Comment