Wananchi wa Burundi leo wanapiga kura ya maoni ya marekebisho ya Katiba.


Wananchi wa Burundi waliotimiza masharti ya kupiga kura leo wanashiriki katika kura ya maoni ya marekebisho ya Katiba ambayo kama itapasishwa itamfungulia njia Rais Pierre Nkurunziza kuiongoza nchi hiyo hadi 2034.
Kura hiyo ya maoni ya marekebisho ya Katiba ambayo kampeni zake zimelalamikiwa na wapinzani wanaosema zilijaa vitisho dhidi ya yao inafanyika siku chache tu baada ya kutokea mauaji makubwa katika mji wa Cibitoke na kuzua wasiwasi mkubwa.
Habari kutoka Bujumbura zinasema kuwa, vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema na kwamba, raia wamejitokeza kwa wingi kwa ajili ya kushiriki katika kura hiyo ya maoni.
Wakati wananchi wa Burundi wakielekea katika masanduku ya kupigia kura leo, mamia ya wapinzani wa Rais Pierre Nkurunziza bado wanaendelea kushikiliwa na hivi karibuni serikali ya Bujumbura ilitangaza kuyapiga marufuku mashirika ya utangazaji ya BBC na VOA pamoja na stesheni mbili za habari za ndani kuendesha shughuli zao nchini humo kwa madai ya kupeperusha taarifa za uongo na zinazotishia usalama wa nchi hiyo.
Hivi karibuni Umoja wa Ulaya ulilaani vikali mchakato wa kuelekea kura ya maoni ya marekebisho ya katiba Burundi ukisema kuwa, unafanyika katika hali ya vitisho na ukandamizaji na kubainisha kwamba, kuendelea kwa mauaji ambayo yanatekelezwa na baadhi ya maafisa wa serikali na watu kukamatwa kiholela bila hatia yoyote ni mambo ambayo hayakubaliki.

Leave a Comment