​Treni 2 TRL Zaacha Njia,Abiria Wanusurika.


Shirika la Reli Nchini (TRL) jana ilieleza ajali ya treni zake mbili ya kawaida na Deluxe zilizotokea Morogoro na Kigoma na kusababisha taharuki kwa abiria zaidi ya 1000 japo hapakuwepo na majeruhi. Mipango ya kuendelea na safari hadi tunaingia mitamboni ilikuwa inakwenda vizuri.

Katika ajali ya Morogoro takribani abiria 857 waliokuwa wakisafiri na treni ya Shirika hilo kutoka Dar es Salaam kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kigoma walipatwa na taharuki baada ya mabehewa saba waliyosafiria kuacha njia ya reli katika eneo la Mazimbu katika Manispaa ya Morogoro.

Aidha treni ya abiria ya mwendo kasi maarufu kama Deluxe iliyokuwa ikifanya safari yake kutoka mkoani Kigoma kuelekea Dar es Salaam imepata ajali katika stesheni ya Nguruka wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma na hivyo kushindwa kuendelea na safari yake.

Akizungumzia ajali ya Morogoro Meneja Mkuu wa Usafirishaji wa TRL, Rashid Ngwani alisema jana mjini Morogoro kwamba treni ya abiria iliyokuwa inakwenda bara ilipata ajali mnamo saa 5:25 usiku wa Mei 12 , mwaka huu katika eneo la Stesheni ya Mazimbu mkoani Morogoro.

Katika ajali hiyo, mabehewa saba yamehusika na manne yakiwa yameegama na matatu yakiwa yameacha njia ya reli. Alisema hakuna madhara makubwa yaliyojitokeza kwa abiria na kwamba utaratibu wa kuwahamishia abiria wote upande wa pili kwa njia ya mabasi aina ya Toyota Coaster ulikuwa umekamilishwa ili kuweza kuendelea na safari yao.

Pamoja na hatua hizo, meneja huyo hakuwa tayari kuzungumzia chanzo cha ajali hiyo ingawa baadaye ilifahamika ni kutokana na athari za mvua, kwani daraja katika eneo husika limetitia.

Mmoja wa abiria katika ajali hiyo alisema walikwama hapo kwa takribani saa nane kuanzia muda wa ajali kabla hawajapatiwa usafiri mbadala wa kuwaondoa katika eneo hilo. Ngwani alisema huduma ya usafirishaji wa abiria kutoka Morogoro kuelekea Kilosa kwa kutumia reli ya kati umesitishwa kwa muda mpaka hapo ukarabati wa eneo ilikotokea ajali hiyo utakapofanyika.

Aliongeza kuwa, abiria waliokuwa wamekwama baada ya mabehewa hayo kupata ajali, walipanda katika mabehewa manne ya nyuma na kurudishwa katika Stesheni ya Morogoro.

Alisema kuwa abiria walikodishwa mabasi aina ya Toyota Coaster na kuwafikisha eneo la kituo cha Lukobe kilichopo karibu na Mazimbu kwa ajili ya kupata treni ya abiria iliyokuwa ikitokea mikoa ya Bara ili waendelee na safari yao na wale wa bara kupanda magari hadi Stesheni ya Morogoro na kuendelea na safari yao kwenda Dar es Salaam.

Naye mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Charles Iyongo mkazi wa mtaa wa Mgudeni , kata ya Mazimbu, Manispaa ya Morogoro alisema kuwa akiwa anaangalia runinga usiku wa saa tano hadi sita alisikia breki kali kwenye njia ya Reli na muda mfupi kusikia kishindo kikubwa.

Alisema eneo hilo ni hatari na korofi kwa kuwa liliwahi kuangusha treni ya mizigo. Wakati huo huo mwandishi wetu akiandika kutoka Kigoma anasema treni ya abiria ya mwendo kasi maarufu kama Deluxe iliyokuwa ikifanya safari yake kutoka mkoani Kigoma kuelekea Dar es Salaam imepata ajali katika stesheni ya Nguruka wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma na hivyo kushindwa kuendelea na safari yake.

Ajali hiyo imetokea jana mchana kilometa moja kutoka stesheni ya Nguruka wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ikiwa ni zaidi ya kilometa 300 kutoka mjini Kigoma ambapo mabehewa manne kati ya mabehewa 12 ndiyo yaliyoacha njia.

Abiria mmoja aliyekuwa akisafiri na treni hiyo, Hussein Seleman alilieleza gazeti hili kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio kuwa zaidi ya mabehewa hayo manne kuacha njia hakuna mtu aliyekufa au kujeruhiwa katika tukio hilo.

Kwa sasa abiria hao wamekwama katika stesheni hiyo ya Nguruka wakisubiri kuinuliwa kwa mabehewa hayo ili safari hiyo iweze kuendelea. Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Ferdinand Mtui akizungumza kwa njia ya simu amethibitisha kutokea kwa ajili hiyo. Na John Nditi, Morogoro; Fadhili Abdallah, Kigoma.

Leave a Comment