Tume Ya Mufti: Wafichueni Waliopora Mali Za Waislamu.


Tume ya Mufti wa Tanzania imewaomba watu wote wenye taarifa au nyaraka zozote kuhusu mali za waislamu, ambazo ziko chini ya usimamizi na umiliki wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), kuziwasilisha kwa tume hiyo, ikiwa ni jitihada za kuunga mkono azma ya Rais John Magufulu ya kurejesha mali za waislamu zilizoporwa kwa hila.

Aidha tume hiyo ambayo ilianza kazi Agosti 10, mwaka huu, inatarajia kuzunguka katika mikoa yote nchini kwa lengo la kuhakiki na kuorodhesha mali za waislamu chini ya Bakwata.

Tume hiyo yenye wajumbe wanane, iliundwa mara baada ya Rais Magufuli kuhutubia Baraza la Idd El Fitri, Julai 6, mwaka huu na kueleza kusikitishwa na hatua ya baadhi ya watu wenye uwezo kutumia mwanya huo kupora mali za waislamu, ambapo aliahidi kuzirejesha.

Wajumbe wa tume hiyo ni Mwenyekiti wake Aboubakar Khalid, Makamu Mwenyekiti Shehe Issa Othman Issa na Katibu wake Salim Abeid. Wajumbe ni Omar Igge, Ali Ali, Taabu Kawambwa, Hamis Mataka na Mohamed Hamis.

Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Shehe Issa alisema Dar es Salaam jana tume inawaomba Watanzania wote wenye taarifa na ushahidi wowote wa ubadhirifu wa mali za waislamu zilizo chini ya usimamizi na umiliki wa Bakwata, kuwasiliana na tume hiyo. Alisema pamoja na mambo mengine, tume hiyo itazifanyia kazi taarifa zozote zitakazowasilishwa kwao na kuwalinda watoa taarifa.

“Tume hii ni huru inaruhusa ya kuendesha kazi zake bila kuingiliwa na mtu au chombo chochote, na inafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na wataalam pamoja na vyombo mbalimbali katika kufanikisha jukumu hilo,” alisema Shehe Issa.

Shehe Issa alisema; “Tume inawaomba waislamu na wapenda heri wote mara itakapofika katika maeneo yao kuipa ushirikiano wa kutosha ili kuiwezesha kufanya kazi hiyo kwa ufanisi, kwani inaamini kwamba jukumu hilo ni zito linalohitaji uaminifu, umakini na weledi wa hali ya juu katika kutekeleza.”

Alisema baada ya Rais Magufuli kutoa ahadi, alimtaka Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakari Zuberi kuunda chombo kitakachofuatilia kadhia hiyo ya mali za waislamu zilizo chini ya Bakwata.

Alisema Mufti kwa mamlaka aliyopewa na Katiba ya Bakwata, Agosti 10, mwaka huu aliunda tume hiyo inayotambulika kama Tume ya Mufti ikiwa na hadidu rejea saba ambazo ni pamoja na kufuatilia suala la misamaha ya kodi mbalimbali zilizoombwa na baraza na taasisi zake nchi nzima.

Kadhalika, alisema tume hiyo itafuatilia mikataba yote ya uuzwaji wa viwanja na mali mbalimbali za baraza na taasisi zake nchi nzima na kuona uhalali wa umiliki huo na kufuatilia mikataba yote ambayo baraza na taasisi zake zimeingia na wawekezaji na kuona mikataba hiyo kama ina maslahi au la.

Shehe Issa alisema tume pia itafuatilia mikataba yote ambayo baraza na taasisi zake zimeingia na wapangaji mbalimbali katika maeneo yanayomilikiwa na baraza na taasisi zake, kufuatilia mali zote za baraza na kuona hali ya usajili wa mali hizo.Alisema pia itafuatilia mapato na matumizi ya baraza na taasisi zake na itapeleka taarifa na mapendekezo yake kwa Mufti ndani ya siku 90 .

Leave a Comment