Chiza: Tanzania ina chakula cha kutosha


Chiiza
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, imesema  Tanzania hivi sasa ina chakula cha kutosha kugawa kwa mikoa yenye upungufu na kuuza nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Waziri wa wizara hiyo, Mhandisi   Christopher Chiza, alisema taifa lina chakula cha kutosha kwa asilimia 118 na kwamba mpaka kufikia Februari 9, mwaka huu, Hifadhi ya Taifa ya Chakula ilikuwa na tani 229,769 zikiwamo tani 226,270 za mahindi na 498.682 za mtama.

Aidha, alisema katika kutekeleza mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, wizara yake imepanga kuanzisha kilimo cha kisasa hasa katika mazao yanayoleta mfumuko wa bei kwa ajili ya kuzalisha zaidi kwa matumizi ya ndani pamoja na kuuza nje.

Katika kufanikisha hilo, Waziri Chiza alisema Wizara imeanza kutekeleza mfumo huo kwenye maeneo  makubwa matatu ikiwa ni pamoja na kuwa na mashamba makubwa ya uwekezaji 25 ya kilimo cha mpunga na miwa, kuwa na skimu za umwagiliaji 78 na maghala 275 ya mahindi.

Alisema lengo ni kuongeza uzalishaji wa mpunga kutoka tani nne hadi nane kwa ekari ifikapo mwaka 2016.

Kwa upande wa uwekezaji katika kilimo, Waziri Chiza  alisema kwa sasa zipo hekta 85,000 ambazo zinatumika kwa kilimo cha uwekezaji na tayari mashamba mawili ya Bagamoyo na Mkulazi mkoani Morogoro yamepata hati.

Kadhalika, alisema tayari Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimeanza zoezi la kutoa mashamba hayo kwa ajili ya kuwekeza.

Aliongeza kuwa wakulima wadogo wametengewa eneo la ekari 3,000 katika mashamba ya sukari  yaliyopo Mkulazi.

Leave a Comment