Ufaransa yasifu mazingira mazuri ya uwekezaji nchini


Dr Reginald-Mengi
Balozi  wa Ufaransa nchini, Marcel Escure ameisifu Tanzania kwa kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji na kuahidi kudumisha ushirikiano na Tanzania katika sekta mbalimbali za uzalishaji.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati alipomtembelea ofisini kwake, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi na kufanya mazungumzo naye kuhusiana na masuala mbalimbali.

Alisema ushirikiano ni lengo namba moja kwa nchi yake kwa nchi za Afrika na kwamba hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila mahusiano mazuri hususani katika uchumi.

Balozi huyo alisema Tanzania imebahatika kuwa na rasilimali nyingi ikiwamo gesi asili na kwamba nchi yake ingependa kuwekeza katika sekta hiyo kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme.

Maeneo mengine aliyosema angependa nchi yake iwekeze ni pamoja na sekta ya usafirishaji na kwamba ili mwekezaji aweze kupiga hatua lazima awekeze katika sekta nyingi badala ya kutegemea moja.

Kwa upande wake, Dk. Mengi alimwambia Balozi huyo wa Ufaransa kuwa, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ambayo anaiongoza haipo kwa ajili ya kuwasaidia wawekezaji wa ndani pekee bali hata wa nje.

Alisema uwekezaji lazima unufaishe pande zote mbili badala ya upande mmoja na kwamba TPSF itahakikisha mazingira mazuri ya uwekezaji nchini yanakuwapo.

Aidha, Dk. Mengi alimuuliza Balozi huyo mpango wa nchi yake kufundisha lugha ya Kifaransa kwa shule mbalimbali hapa nchini.

Akijibu, Balozi Escure alisema mpango huo  upo na kwamba wameanza kufanya mazungumzo na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na kutoa mafunzo mbalimbali.

Aidha, Dk. Mengi alitaka kujua namna Ufaransa ilivyojipanga kuwasaidia wakulima hapa nchini kwa kununua mazao yao.

Balozi huyo alimhakikishia Dk. Mengi kuwa wakulima wa Tanzania wanaotaka kuuza mazao yao nchini mwake wanakaribishwa na kwamba hakuna vikwazo.

Leave a Comment