Warioba: Acheni kuwafundisha wananchi cha kusema Katiba mpya


                           Mwenyekiti wa Tume ya Mabadaliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba

Mwenyekiti  wa Tume ya Mabadaliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, amewataka viongozi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia, vikundi vya kidini na wanaharakati kutowafundisha wananchi maoni ya kuchangia kwenye mikutano ya tume kwa kuwa wana mawazo yao huru na wanajua nini wanachotaka kiingizwe kwenye katiba mpya.

Jaji Warioba aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kuwapatia mrejesho wa mikutano iliyofanywa na tume yake kwa kipindi cha mwezi mzima katika mikoa minane waliyoitembelea ya Pwani, Dodoma, Manyara, Kagera, Shinyanga, Tanga, Kusini Unguja na Kusini Pemba, katika awamu ya kwanza ya ziara yao ya kukusanya maoni.

Jaji Warioba alisema kwamba moja ya changamoto kubwa waliyokumbana nayo kwenye ziara yao ya awamu ya kwanza, ni ya vyama vya siasa na makundi mengine ya kijamii kuingilia uhuru wa wananchi wakati wa kutoa maoni.

“Vyama vya siasa vimekuwa vikitoa kauli na maelekezo kwa wanachama wao ili wafuate misimamo ya vyama, jambo ambalo linawanyima uhuru wa kutoa maoni yao. Ni rahisi kugundua kwamba wananchi wameelekezwa kutoa maoni na vyama au vikundi fulani kwenye mikutano yetu,” alisema Jaji Warioba.

Alifafanua kwamba haiwezekani wananchi wote wa Mkoa wa Kagera kwa mfano kila anayesimama kuchangia maoni anakuwa na pendekezo sawa na la mwenzake na anapoombwa kulifafanua pendekezo lake anashindwa, wakati anapotoa maoni yake mwenyewe yasiyo ya kutumwa anaweza kuyafafanua vizuri zaidi.

Jaji Warioba aliyaasa makundi hayo kuwaacha wananchi wautumie muda wao kwa ukamilifu bila ya kuwashinikiza, kwa kuwa pamoja na kutojua yaliyo ndani ya Katiba iliyopo, lakini bado wameweza kutoa maoni yanayoashiria Tanzania wanayoitaka ambayo yaligusa kwenye maeneo ya ardhi, kilimo, elimu, afya, hifadhi ya jamii na mfumo wa uongozi na utawala.

Alisema kuwa wananchi pia waligusia masuala ya Bunge, Mahakama, misingi ya kitaifa, madaraka ya wananchi na mengine.

MWITIKIO MKUBWA

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, wakati wa ziara hiyo kulikuwa na mwitikio mbukwa kutoka kwa wananchi.

Alisema kuwa jumla ya mikutano 386 ilifanyika katika mikoa yote minane waliyotembelea, minane kati ya hiyo ilihusisha makundi maalumu, zikiwemo taasisi za dini na vyombo vya ulinzi na usalama.

Jaji Warioba alisema kwa wastani wa wananchi 188,679 walihudhuria mikutano ya tume, ikiwa ni wastani ya watu 489 kwenye kila mkutano hali inayoonyesha mwamko wa wananchi wa kutoa maoni.

Alisema jumla ya wananchi 17,440 walitoa maoni kwa njia ya kuzungumza kwenye mikutano na jumla ya wananchi 29,180 walitoa maoni yao kwa njia ya maandishi na kuyawasilisha kwenye mikutano ya tume.

Akizungumzia awamu ya pili ya ziara ya ukusanyaji wa maoni ya wanannchi inayofuata, Jaji Warioba alisema kwamba itaanza rasmi Agosti 27 na kukamilika Septemba 28, mwaka huu.

“Tutatembelea mikoa saba ambayo ni Mbeya, Morogoro, Lindi, Ruvuma, Kigoma, Katavi na Mwanza,” alisema.

Tume hiyo yenye wajumbe 30 wakiwamo 15 kutoka Zanzibar na 15  Tanzania Bara, ilianza kazi Mei 15, mwaka huu.

Ukusanyaji wa maoni ni hatua ya mwanzo ya mchakato wa kuandika katiba mpya ambayo inatarajiwa itumike kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Baada ya maoni kuchmbuliwa na ripoti kuwasilishwa kwa Rais, atawasilisha mapandekezo kwenye mkutano wa Bunge la Katiba, kisha kuandaliwa kwa katiba ambayo itawasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya kura ya maoni kama inakubalika au la.

CHANZO: NIPASHE

Leave a Comment