Maafa tena


 

  17 wafa papo hapo,78 majeruhi
 
Basi la Sabena aina ya Scania lenye namba za usajili T 570 AAM, lililopata ajali na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 78 kujeruhiwa.

Watu 17 wamefariki dunia na wengine 78 kujeruhiwa wanne kati yao vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Tabora kwenda Mbeya kupinduka eneo la Kitunda Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.

Majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Kitunda na jitihada za kuwahamishia katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete kwa matibabu zaidi zilikuwa zikiendelea lakini abiria 54, kati yao, walitibiwa na kuendelea na safari yao baada ya kufanyiwa uchunguzi na kubainika kuwa hawakuwa na majeraha makubwa.

Ajali hiyo ilihusisha basi la Sabena aina ya Scania yenye namba za usajili T 570 AAM.

Miongoni wa watu walikufa ni watoto watano, wanawake sita na wanaume sita ambao miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa Kitete kwa ajili ya kutambuliwa na ndugu na jamaa zao.

MAITI SABA ZATAMBULIWA

Hata hivyo, hadi kufikia jana mchana, miili ya watu saba ilikuwa imetambuliwa na baadhi ya ndugu. Waliotambuliwa ni pamoja na askari Polisi PC Kheri wa Kituo Kikuu Kikuu cha Polisi cha mjini Tabora; Vitus Tulumanye, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) tawi la Tabora; Farah Inga; raia wa Zimbabwe aliyekuwa akifanya kazi Tabora; Ikamba Thadeo; Damalu Goma;  Beatrice Kalinga, mwalimu wa Shule ya Msingi Igoko wilayani Uyui mkoani Tabora na aliyetambuliwa kwa jina moja la Madirisha ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi katika Wilaya ya Kaliua.

Mwalimu Madirisha anadaiwa alifuatana na watoto wanne na mkewe ambao bado hawajatambuliwa.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na dereva wa basi hilo ambaye amenusurika katika ajali hiyo, chanzo chake ni lori aina ya Fuso lililokuwa limeegeshwa katika kona, hivyo dereva alipojaribu kulikwepa usukani ulikatika na hivyo basi hilo likaacha njia na kupinduka.

Dereva huyo, Ali Nassoro, alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 6:30 mchana na kufafanua kuwa walishindwa kutoa taarifa mapema kutokana na eneo walilopatia ajali kutokuwa na mawasiliano ya simu za mkononi.

Hata hivyo, alisema walimpata mtu aliyekuwa anakwenda Sikonge na kumwagiza akatoe taarifa za ajali hiyo.

BAADHI YA MAJERUHI

Baadhi ya majeruhi wametambuliwa kwa majina ya Grace Mbunga, Kayungilo Nsungu, Zena Shigela, Ndisi Ngosha, Kulwa Kija, Feni Salum, Shinje Kayogole na Emmanuel Charles.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Anthony Rutta, alitibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwataka abiria wanaotumia usafiri wa mabasi kutoa taarifa mara moja baada ya kuona basi ambalo wanasafiri nalo limejaa kupita kiasi.

Kamanda Ruta alisema basi la Sabena lililopata ajali lilikuwa limebeba zaidi ya abiria 110.

Alisema dereva wa basi hilo alitiwa mbaroni kwa tuhuma za kusababisha ajali hiyo na anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya taratibu kukamilika.

MWANAJESHI AWALAUMU POLISI

Askari mmoja wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Shabani Mtawazi, alilirushia lawama Jeshi la Polisi hasa Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya mabasi yanayokiuka sheria za usalama barabarani.

Mtawazi aliyekuwa abiria wa basi hilo, alisema tangu walipoondoka mjini Tabora, walikaguliwa na askari wa usalama barabarani na kutoa malalamiko kwamba basi lilikuwa kwenye mwendo wa kasi lakini hakuna hatua zozote zilichukuwaliwa na askari hao.

 Askari huyo wa JWTZ alisema dereva huyo alikuwa katika mwendo kasi, lakini licha ya abiria kulalamika, askari hao hawakuchukua hatua zozote hali iliyosababisha watu wengi kupoteza maisha yao na wengine kujeruhiwa.

Katibu Tawala ya Mkoa wa Tabora, Kurda Mwinyimvua, aliongoza kusimamia zoezi la kutoa huduma ya kwanza kwa majeruhi katika eneo la tukio takriban kilomita 200 kutoka mjini Tabora.

Mwinyimvua alikwenda eneo la tukio akiwa ameongozana na uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Tabora ambao walipeleka wauguzi na dawa kwa ajili ya kuokoa maisha ya majeruhi.

 

CHANZO: NIPASHE

2 Comments

 1. SANKY says:

  I was very touched with this accident as I heard that our lovely Aunt was involved. We were waiting for her come-back, but she couldn’t manage to reach us. We’ve extremely mourned for her. Every morning when we wake up, we remember the good things she used to do, and how friendly she was to others. We don’t know if we will get another person as she was.Thus, we’ll never forget her, and her name will be our daily song. May her Soul Rest in Peace for ever and ever.
  With bitter tears,

  My name is Sanky.

  • admin says:

   Dear Sanky,
   We are extremely sorry for your loss, we send our condolences to you and your family. Our prayers are with her, May her soul rest in peace. Ameen

Leave a Comment