Mazoezi ya Kijeshi ya Russia katika Bahari ya Mediterranean


Mazoezi ya Kijeshi ya Russia katika Bahari ya Mediterranean

Sambamba na kushadidi mashinikizo ya nchi za Magharibi dhidi ya Syria na kuendelea uungaji mkono wa kivitendo wa Moscow kwa serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria, Russia imetuma meli zake za kivita katika kituo chake cha kijeshi katika Bandari ya Tartus nchini Syria. Aidha Russia imesema itafanya mazoezi ya kijeshi katika Bahari ya Mediterranean.
Imeripotiwa kuwa, meli hizo za kivita za Russia zitabakia katika Bahari ya Mediterranean kwa muda wa miezi mitatu.

Hata kama Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa mazoezi ya kijeshi ya nchi hiyo katika Bahari ya Mediterranean yalikuwa yamepangwa tokea huko nyuma, lakini weledi wa mambo wanasema kutumwa manowari za Russia katika Bandari ya Tartus ni jambo linaloashiria azma ya viongozi wa Moscow ya kuendelea kuiunga mkono kivitendo serikali ya Rais Bashar al Assad. Kimsingi ni kuwa Russia inataka kutuma ujumbe wa wazi kwa Marekani na waitifaki wake kuwa, Moscow ina azma imara ya kulinda maslahi yake katika eneo.
Katika upande mwingine jeshi la Syria limefanya mazoezi makubwa yaliyojumuisha vikosi vya nchi kavu, angani na baharini. Mazoezi hayo ya jeshi la Syria yametajwa kuwa ni jibu la kivitendo kwa vitisho vya nchi za Magharibi ambazo zinafikiria kuivamia kijeshi Syria.
Kilichowazi ni kuwa hatua ya Russia ya kutuma meli kadhaa za kivita katika Bahari ya Mediterranean na kutia nanga katika Bandari ya Tartus nchini Syria, sambamba na kufanyika mazoezi makubwa ya jeshi la Syria si mambo yaliyofanyika kwa sadfa. Inaelekea kuwa, kwa upande moja, serikali ya Syria kwa mazoezi hayo ya kijeshi imeonyesha azma yake ya kukabiliana na hujuma yoyote ya maadui na kwa upande wa pili hatua ya Russia ya kutuma manowari zake nchini Syria ni onyo kali kwa nchi za Magharibi kuwa Moscow iko tayari kabisa kulinda maslahi yake nchini Syria.
Viongozi wa Russia wanafahamu vyema kuwa iwapo serikali ya Syria itaangushwa kupitia hujuma ya kijeshi ya nchi za Magharibi, uhusiano wake na Damascus utavurigika. Aidha kwa mtazamo wa kiuchumi na kijeshi, Russia itapata hasara kubwa iwapo Syria itakuwa kibaraka wa Magharibi kwani mbali na kupoteza soko lake la silaha huko Syria, jeshi la wanamaji la Russia pia litatimuliwa katika bandari ya kiistratejia ya Tartus.
Ni kwa sababu hii ndio maana Russia na China zikiwa wanachama wawili wa kudumu wa Baraza la Usalama zimekuwa zikitaka mgogoro wa Syria utatuliwe kwa njia za amani. Wakuu wa Russia wamesisitiza mara kadhaa kuwa katika makubaliano yoyote ya kitaifa ya kutatua mgogoro wa Syria ni lazima makundi ya waasi yaweke chini silaha. Aidha Russia imetaka uungaji mkono wa kigeni kwa waasi usitishwe mara moja na mkondo wa marekebisho ulioanzishwa na serikali ya Syria uendelee. Msimamo huu wa Russia unapingwa vikali na maadui wa serikali ya Syria hasa Marekani na waitifaki wake Ulaya na katika baadhi ya nchi za Kiarabu. Kinachojitokeza wazi ni kuwa, pamoja na kuwepo mashinikizo ya nchi za Magharibi, Russia ina azma ya kuendelea kuiunga mkono kikamilifu serikali ya Syria. Hakuna shaka kuwa mgogoro wa Syria sasa umegeuka na kuwa vita vipya baridi duniani.

Leave a Comment