Zitto apinga matumizi ya teknolojia ya GMO


                                      Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe

Mbunge  wa Kigoma Kaskazini (Chadema),  Zitto Kabwe, amepinga matumizi ya teknolojia ya Uhandisi jeni ambayo huzalisha Genetically Modified Organisms (GMO), kwa sababu unawarudisha Watanzania katika ukoloni mambo leo na mikono ya mabeberu.

Zitto alisema hayo bungeni jana, wakati akichangia hotuba ya makadirio ya matumizi na mapato ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa mwaka 2012/13. “Nimeshtushwa na Serikali kuona namna sasa hivi tunavyopigia debe GMO na Serikali kuzungumza bila uoga, nchi hii sasa bila aibu tunapigia debe GMO,”alisema na kuongeza kuwa:

“ GMO inaturudisha katika ukoloni, itatufanya tuwe tegemezi, hatupingi maendeleo ya Sayansi, hatupingi utafiti, tunapinga nchi yetu na wakulima wetu kutegemea mbegu kutoka katika makampuni makubwa.”

Alisema ameona jinsi kampuni ya kuzalisha mbegu ya Monsanto inavyoshiriki katika kila hatua katika kilimo kwanza, jambo ambalo kukubaliana nalo ni kuliingiza taifa katika utegemezi.

“Mheshimiwa Naibu Spika kama nchi yetu imefikia mahali tunakubali GMO, tukubali tunaenda kwenye tegemezi. Sisi hatuna uwezo wa kuzalisha mbegu kama makampuni makubwa yanavyofanya, badala ya kumwezesha mkulima wetu awe na mbegu zetu sasa tunafanya mbegu zinaenda kununuliwa dukani.”

Alisema yeye haungi mkono matumizi ta teknolojia hiyo kwa kuwa ni ukoloni na inalirudisha taifa kwenye mikono ya mababeberu.

Pia aliwataka watanzania wote kumuunga mkono kwa kupinga matumizi ya teknolojia hiyo.

Awali akisoma hotuba yake ya bajeti, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alisema GMO katika kilimo inaweza kuongeza ubora na uzalishaji wa mazao ya kilimo, kupunguza gharama za uzalishaji, kuhifadhi mazingira na kwa kupunguza matumizi ya madawa na mbolea, kusafisha mazingira na uzalishaji wa nishati mbadala.

Aliyataja madhara hayo kuwa ni pamoja na uharibifu wa bayoanuai na uoto wa asili na uchavushaji wa mazao na mimea mingine, utegemezi wa kampuni chache, ongezeko la sumu na mzio, uharibifu kwa viumbe ambavyo havikukusudiwa, kuongezeka kwa magugu na kuibuka kwa visumbufu na magonjwa sugu.

Kwa upande wake Kamati ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, ilisema matumizi ya teknolojia ya GMO, bado hayajatiliwa mkazo.

 

CHANZO: NIPASHE

Leave a Comment