Duru mpya ya mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza na jibu la Wapalestina


Kumekuwepo habari za kuendelea kwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza. Jana usiku ndege za kivita za utawala haramu wa Israel ziliyashambulia maeneo ya miji wa Rafah na Khan Yunus yaliyoko katika ukanda huo wa Ghaza.

Jumapili iliyopita askari wa utawala huo wa Kizayuni walilishambulia eneo la Deir al-Balah lililopo mashariki mwa ukanda huo na kuwajeruhi watoto watano wa Kipalestina. Kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Ghaza kunakuja wakati ambao siku chache zilizopita serikali halali ya Palestina inayoongozwa na Ismail Hania ilitangaza kuwa, mwezi uliopita wa Juni kulirekodiwa mashambulizi yapatayo 58 yaliyofanywa na ndege za kivita na vifaru vya utawala haram wa Israel dhidi ya ukanda huo, ambapo Wapalestina 19 waliuawa shahidi na wengine 70 kujeruhiwa.
Makundi ya kupigania uhuru ya Kipalestina yamejibu mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel dhidi ya ukanda huo, kwa kuvurumisha makombora kuelekea maeneo ya Wazayuni huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Aidha hapo jana makundi ya muqawama yalivurumisha roketi moja katika eneo la Eshkol la kusini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Kabla ya hapo Brigedi ya Izzudin Qassam, tawi la kijeshi la harakati ya Hamas liliuonya utawala wa Kizayuni kuwa, jinai zozote zitakazotekelezwa dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza, zitajibiwa kwa radiamali kali kutoka kwa wanamapambano hao.
Naye Ismail Haniya Waziri Mkuu wa serikali halali ya Palestina amesisitiza kwamba, Wapalestina wamekuwa wakifungamana na misingi pamoja na haki zao na kwamba hawatorejea nyuma kuhusu suala hilo.
Mashambulizi na jinai kadhaa za utawala huo dhidi ya maeneo ya Kipalestina, hata kama yamewaathiri vibaya Wapalestina, lakini masaibu hayo hayajapelekea hata chembe kulegea wala kutiwa doa irada yao ya kupigania matukufu yao. Katika hali kama hiyo fikra za waliowengi duniani zinasubiri kuona, jamii ya kimataifa ikifanya juhudi za dhati za kuwasaidia raia hao wasio na mtu wa kuwatetea sambamba na kuchukuliwa hatua za kweli zitakazolinda haki zao. Hii ni kwa sababu hadi sasa jamii hiyo bado haijachukua hatua zozote za maana kwa ajili ya kusitisha jinai za utawala wa Kizayuni huko Palestina. Nukta hiyo imechangia pakubwa katika kuishajiisha Israel iendelee kutekeleza jinai tofauti dhidi ya raia wa Palestina. Aidha mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza yanakuja katika hali ambayo siku kadhaa zilizopita kutokana na woga wa kushadidi kwa mashambulizi ya muqawama dhidi yake, utawala wa Israel ulilazimika kutia saini ya usitishwaji mapigano na Wapalestina. Lakini kama kawaida yake, utawala huo umepuuza ahadi zake za hivi karibuni kwa Wapalestina na kuanza tena kuushambulia kinyama Ukanda wa Ghaza.

Leave a Comment