SIKU YA MIIRAJ NA BI’ITHAH


SIKU YA MIIRAJ NA BI’ITHAH

TOLEO LA IJUMAA Na. 14

24.Rajab 1433AH/15 June 2012

Jumatatu ijayo ni sawa na mwezi 27 Rajab.Hii ni siku muhimu sana katika historia yetu ya kiislamu,kuna matukio mawili makubwa yanayomuhusu mtume wetu Muhammad (saww) ambayo yametokea katika siku kama hii.Tukio la kwanza ni tukio linalofahamika kama bi’ithah,yaani tukio la kutawazwa rasmi Bwana Mtume (saww) kuwa mtume,tukio hili lilitokea katika siku kama hio mwaka 610 A.D(baada ya kuzaliwa Nabii Isa(AS).Tukio la pili ni tukio la Israa na Miiraj(safari ya Bwana Mtume (saww) kutoka Makkah hadi Jerusalem(Palestine iliyokaliwa) na kutoka Jerusalem hadi mbinguni).Bila shaka matukio yote mawili ni matukio makubwa nay a muhimu ambayo si busara yatupite kimyakimya bila ya kusimama na kuyazingatia kidogo,ndipo tukaona tushirikiane kwa njia hii ya makala.

  • TUKIO  LA BI’ITHAH:

 

Kama tulivyoelezea hapo juu kuwa tukio la bi’ithah  ni tukio la kutawazwa kwa mtume wetu kuwa ni mtume,kuna ibara inayotumika kuelezea tukio hili ambayo si sahihi,nayo ni ibara inayoelezea tukio la bi’ithah  kwa maana ya tukio la bwana mtume (saww) KUPEWA UTUME.Maelezo haya si sahihi kwa sababu Bwana Mtume (saww) hakupewa utume alipokuwa na umri wa miaka 40 (tukio la bi’ithah lilipotokea) sawa ni kuwa alizaliwa akiwa ni mtume ila aliamrishwa kuanza kazi ya utume(assignment) alipofikisha umri wa miaka 40.Twaweza kufananisha fikra hii na uongozi wetu wa kisiasa,rais anapochaguliwa kwa kura anakuwa ni rais mteule(president elect)lakini hawezi kutekeleza majukumu ya kirais hadi atakapoapishwa,anapoapishwa haina maana ndiyo anapewa urais ,urais alishapewa kwa kura za wananchi.Mwenyeezi Mungu alikwishamchagua Muhammad awe ni mtume wa mwisho kabla hajamuumba Nabii Adam(as).

عن أبي هريرة قال:قالوا:يا رسول الله,متى وجبت لك النّبوّة؟قال:”و ادم بين الرّوح و الجسد”

“Imepokewa kutokana na Abuhurairah kuwa amesema:Walisema(maswahaba),ewe Mtume wa Mwenyeezi Mungu lini uliwajibikiwa na utume?Akasema(mtume):wakati Adam(as) yu kati ya roho na mwili”

SWAHIIH TIRMIDHIY,Baabu fadhli nnabiy.

Yaani Bwana Mtume (saww) tayari alishakuwa ni mtume wakati Adam(as)hajakuwa mtu kamili.

  • Tukio lenyewe:

Kabla ya Bwana Mtume (saww) hajatawazwa rasmi kuwa ni Mtume alijipambanua kwa mambo mengi na jamii iliyomzunguka,hakupata kusujudia masanamu wala kuyaheshimu kwa namna yoyote,bali alikiyachukia,Hakupata kunywa pombe wala kufanya uchafu wowote katika uchafu wa kijaahiliyyah,mpaka akawa anafahamika kwa jina la Asswaadiqul Amiin(mkweli muaminifu).Alikijuwa kuwa hawa watu wamepotea lakini alikuwa hajaamrishwa kulingania,ndipo akaamua kujitenga akawa anakwenda nje katika majabali kwenye pango la Hiraa,alikuwa akichukua chakula chake na mahitaji yake mengine na akikaa huko akimuabudu Mwenyeezi Mungu na akifikiria juu ya utukufu wake.Siku moja wakati yumo humo pangoni akajiliwa na malaika mtukufu Jibril,Akamwambia soma mtume akamwambia mimi sijui kusoma mara tatu Jibril akimwambia asome na yeye  akijibu mimi sijui kusoma,ndipo akamsome aya 7 za mwanzo za suratul Qalam(IQRAA),kisha mtume akarudi zake Makkah.Kwa ufupi hivi ndivyo ilivyokuwa.

Lakini kwa kuwa tukio hili la bi’itha ni tukio la kihistoria,na kama tujuavyo historia mara nyingi ina tofauti kila mmoja aeleza kivyake(historia ni neno lenye asili ya kiingereza history,ni mpandamanisho wa maneno mawili his story yaani riwaya yake, yaweza iwe kweli au uongo.),kuna mambo yaliyopachikwa katika tukio hili ambayo si ya kweli hata kama yamo katika vitabu vya waislamu(tusiamini kila lililomo kitabuni kwani vimeandikwa na watu,Qur’an peke yake ndiyo kitabu kisicho na shaka ndani yake).Miongoni mwa mambo hayo ni madai kuwa eti Bwana Mtume (saww) hakujua kuwa yule aliemjia kule pangoni ni malaika yeye alidhani ni jini na kwamba yale aliyoyaona ni mambo ya majini,na wengine wakafikia kudai kuwa kwa jinsi alivyochanganyikiwa alitaka kwenda kujirusha juu ya  mlima afilie mbali(Soma Taareikh Twabariy).Akarudi kwa mkewe Khadija akamuelezea aliyoyaona ,mama Khadija(as) akamchukua kwa binami yake Waraqah bin Nawfal aliekuwa ni mkristo.Waraqah  baada ya kuelezewa aliyoyaona akamwambia usiogope uliemuona sio jini wala shetani bali ni malaika aliekuwa akiwajia mitume wote waliopita na kwamba wewe ni mtume sasa.

 

  • Mtazamo wetu:

Sisi hatuikubali riwaya hii kwa sababu:

i-haiwezekani kwa Mwenyeezi Mungu kumpa mtu utume hali yule aliyepewa utume hajui kuwa yeye ni mtume

ii-Vipi mtume wa Mwenyeezi Mungu ambae ndiye bora wa mitume wote,mtume ambae ndiye atakaetimiza ndoto za mitume waliomtangulia katika dunia asijijue kuwa yeye ni mtume mpaka atake kujiua?

iii-yawezekana vipi mtume mwenyewe asijijue kuwa ni mtume mpaka aambiwe na mtu mwingine asiekuwa ni mtume?

 

  • Ukweli ni upi?

Kwa hakika haijapata kutokea katika historia ya mitume wote waliotangulia kwamba mtume fulani kapewa utume na hali ya kuwa yeye mwenyewe hajui mpaka aambiwe na mtu mwingine,hayakutokea kwa Isa wala kwa Musa wala kwa yeyote miongoni mwa mitume(amani iwe juu yao).Ikumbukwe kuwa Mtume Muhammad ndiye Sayyidul anbiyaai walmursaliina(bwana wa mitume yote).Vipi  bwana wa mitume yeye mwenyewe asijue kuwa ni mtume mpaka ende akaambiwe na mkristo ,usiogope wewe ni mtume?Inaingia akilini kweli?Katika Quran Mwenyeezi Mungu(swt)amwambia mtume wake Muhammad aseme:

 

“Sema, hii ndiyo njia yangu nalingania kwa Mwenyeezi Mungu kwa ujuzi kamili mimi na wale walionifuata

(Surat Sabai:108).

 

Kwa kuwa sisi  hatukuwepo wakati huo ni lazima tupate rejea ya mtu aliekuwepo wakati huo.Kwa sababu riwaya tuliyotangulia kuitaja katika kitabu cha Musnad  Ahmad imepokewa kutokana na Mama Aisha (r.a)ambae hakuwepo wakati huo bali alikuwa hajazaliwa kamwe!Lakini Imam Ali bin Abitwalib(as) ni mtu wa karibu mno na Bwana Mtume (saww) na kwa hakika huwezi kuandika historia ya kiislamu bila ya kumtaja Imam Ali(as),hata Bwana Mtume (saww) alipokuwa akienda pangoni alikuwa akiongozana  naye.Akielezea uhusiano wake na Bwana Mtume (saww) anasema:

“N a kwa hakika mwajua nafasi yangu kwa Bwana Mtume (saww) kwa undugu wetu wa karibu na daraja maalum (niliyokuwa nayo kwake),aliniweka mapajani mwake ningali mtoto mdogo, akinilaza katika tandiko lake na akinigusisha mwili wake,akininusisha harufu yake na alikuwa akitafuna kitu kisha akinipa nimeze”

 

Akaendelea kusema:

“Na kwa hakika alimuekea (Muhammad)Mwenyeezi Mungu malaika mkubwa kabisa miongoni mwa malaika wake tangu alipoacha kunyonya(kwa ajili ya kumfundisha)……na alikuwa akienda katika pango la hiraa kila mwaka na alikuwa haonekani na yeyote ila mimi tu.N a nilisikia ukulele(siku ya bi’ithah) nikamuuliza ni ukelele gani huu?Akasema .huyo ni shetani amekata tamaa na kuabudiwa”

 

Alkhutbah al-qaaswi’ah,Nahjul Balaghah.

 

Kwa maneno haya ya Imam Ali(as) twafahamu kuwa Bwana Mtume (saww) mara tu alipoacha kunyonya Mwenyeezi Mungu alimuekea malaika wa kumfunza mambo mbalimbali,vipi afikishe miaka 40 na hajajua kuwa yeye  ni mtume?Halikadhalika Imam Ali(as) atueleza kuwa siku ile mtume alipotawazwa kuwa mtume Iblis alipiga ukulele wa masikitiko,vipi Iblis ajue kuwa leo Muhammad ametawazwa kuwa Mtume mtume mwenyewe asijue?

Mwisho lau Muhammad(saww)angelikwenda kwa Waraqah mkristo bila shaka Imam Ali angejua na angetuelezea ,kulinyamazia jambo hili ni dalili kuwa halikuwepo na hata Mama Aisha(ra) amesingiziwa tu,hakuyasema hayo,hizi ni riwaya za kiyahudi zilizochomekwa katika vitabu vya waislamu kumteremsha cheo mtume wetu.

  • ANGALIZO:

Kuna baadhi ya wenye chuki wanaodai kuwa imani ya Shia ni kwamba Utume ulikuwa ni wa Ali(as) lakini Jibril(as)akafanya khiana(twajikinga kwa Mwenyeezi Mungu na maneno hayo)akampa Muhammad (saww) badala ya Ali(as).

Jawabu:Jawabu zuri kwa watu hao ni kuwaombea kwa Mwenyeezi Mungu(swt) aondoshe chuki katika nyoyo zao,na afungue vifua vyao,awape elimu ya yale walo na ujinga nayo,Rabbi twakuomba dua hii ikubali kwa haki ya Muhammad na kizazi chake ,Aamin.

 

Wiki ijayo:Safari ya Israa na Miiraj.

 

Imetolewa na

Bilal Muslim Mission-Tanga Beanch

E-mail:abuzahraa22@yahoo.com

P.O.Box 555  Mob:0713837529

TANGA.

 

Leave a Comment