5 Shaaban 1433, 25 Juni 2012


Leo ni Jumatatu tarehe 5 Shaaban mwaka 1433 Hijria sawa na tarehe 25 Juni 2012 Miladia
Siku kama ya leo miaka 1395 iliyopita mwafaka na tarehe 5 Shaaban mwaka 38 Hijria Ali bin al Hussein, mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu wa Uislamu (s.a.w) alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na kutokana na kuwa pamoja na baba yake yaani Imam Hussein (a.s) mjukuu wa Mtume Muhammad (s.aw), mtukufu huyo alipata mafunzo mema ya kimaanawi na kiaklaqi na kunufaika na mafunzo ya bahari kubwa ya elimu ya baba yake. Mtukufu Ali bin al Hussein (a.s) alisifika kwa takwa na kumcha Mwenyezi Mungu kwani alikuwa akikesha usiku kwa ajili ya ibada. Alipewa lakabu ya Sajjad yaani mtu anayesujudu sana kutokana na sijda zake za muda mrefu alizokuwa akizifanya kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu SW.
Miaka 1120 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia tabibu na mwanakemia mtajika wa ulimwengu wa Kiislamu na mvumbuzi wa alkoholi kwa jina la Muhammad bin Zakaria Razi. Tabibu Razi alizaliwa mwaka 251 Hijria katika mji wa Rei kusini mwa Tehran ya leo. Mwanakemia huyo mkubwa alianza kujishughulisha na kazi ya usonara na baadaye kemia. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa. Baadae Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya Sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia. Msomi huyo wa Kiislamu Muirani alikuwa shakhsia wa kwanza kuvumbua alkoholi.
Na siku kama ya leo miaka 190 iliyopita kundi la watumwa weusi wa Marekani ambao walikuwa wameachiwa huru na wamiliki wao wazungu lilirejea Afrika na kuweka makazi yao katika ardhi inayojulikana hii leo kwa jina la Liberia. Raia weusi wa Marekani walianzisha mapambano tangu mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia lengo likiwa ni kujiondoa katika utumwa wa wazungu na kuasisi nchi kwa ajili ya raia weusi. Rais wa kwanza wa Liberia alikuwa Joseph Jenkins Roberts ambaye alikuwa mtumwa kutoka jimbo la Virginia.

 

Leave a Comment