Migiro awataka Watanzania kuchapa kazi kwa nidhamu


Naibu 0Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha-Rose MigiroNAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha-Rose Migiro amewaasa Watanzania kufanya kazi kwa bidii na nidhamu kupata mfanikio katika sekta yoyote ile.

Amesema hakuna jambo njema katika utumishi wowote ule uwe wa kuajiriwa serikalini ama sekta binafsi au hata kujiajiri mwenyewe kama utafanya kazi kwa bidii na nidhamu.

Migiro alitoa kauli hiyo wakati akisalimiana  na Watanzania waliopo New York,  Washigton DC na vitongoji vingine wakati wa hafla ya kusherehekea mafanikio yake ya kushika wadhifa wa Unaibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Miaka mitano na nusu.

Hafla hiyo iliandaliwa kwa ushirikiano wa Jumuiya za Watanzania waliopo hapo na  Balozi za Tanzania nchini Marekani na Umoja wa Mataifa.

Katika hafla hiyo iliyofanyika katika makazi ya Balozi wa Tanzania New York, Migiro alisema hata yeye asingefika hapo alipo au hata asingemaliza miaka hiyo mitano na nusu kama asingeonyesha nidhamu ya hali ya juu katika kazi.

“Tumekusanyika hapa kusherehekea mafanikio haya, haya si mafanikio yangu binafsi ni mafanikio  yetu  sote, ni mafanikio ya nchi yetu ni mafanikio ya Bara la Afrika. Lakini nimefika hapa nilipo pamoja na mambo mengine ni suala la nidhamu, nidhamu ile tuliyofundishwa zamani mashuleni. Kwa sababu hiyo  ninawaomba na nyie muweke mbele nidhamu katika kazi na shughuli zenu” alisisitiza, Dk Asha- Rose Migiro.
Aidha Migiro anasema kwamba utumishi wenye  kuweka mbele nidhani si jambo geni kwa sababu ni nidhamu hiyo hiyo iliyoonyeshwa na viongozi waasisi wa Taifa la Tanzania , waliopita na waliopo ndiyo imeifanya Tanzania kuwa kama ilivyo na kutambulika  kimataifa.

“Tumefika hapa, kwa sababu viongozi wetu walifanya kazi kwa  nidhamu sana, wakafyeka misitu na mapori, wakaua  majoka,  kazi ambayo imetuwezesha sisi kupita na kufika hapa tulipo” alisititiza.
Katika mazungumzo hayo ambayo mara kwa mara yalikuwa yakibwagizwa  kwa  “Tanzania Oyeee”, Naibu Katibu Mkuu, pia aliwataka Watanzania kudumisha amani, upendo, mshikamano na umoja.

Alisema kwamba katika nafasi yake ya unaibu katibu mkuu, ameyaona mengi, ameyasikia mengi kiasi cha kumfanya  aienzi amani na mshikamano walionao Watanzania.

Awali akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu kuwasalimia Watanzania, Balozi wa Tanzania  nchini Marekani, Mwanaidi Maajar  alimuelezea Migiro kama kiongozi mwanamke  na mama ambaye  amekuwa kivutio kikubwa kwa wanawake wengi kwamba hata wao wanaweza kuja kuwa  kama Migiro.

 

Leave a Comment