Fedha za tumbaku zinufaishe familia-DC


WAKULIMA wa zao la tumbaku wilayani hapa, wameshauriwa kutotumia fedha za mauzo ya tumbaku kuongeza wanawake badala yake wajikite katika kupanga masuala ya maendeleo kwa familia zao.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Fatma Taufiq alitoa ushauri huo kwenye sherehe za ufunguzi wa soko la tumbaku lililofanyika kiwilaya katika kijiji cha Mitundu.

Fatma, ambaye hiyo ilikuwa ziara yake ya kwanza wilayani tangu alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni, alisema uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya wanaume wamekuwa wakihama familia zao mara tu baada ya mauzo ya tumbaku.

Alifafanua akisema kuwa japokuwa hiyo si tabia ya wanaume wote, lakini umefika wakati kwa wale wenye kujali familia zao, kuwashauri wenzao waachane na hasara na taabu wanazopata baada ya kuishiwa mapato yatokanayo na mauzo ya tumbaku.

“Kwa kweli nawashauri wanaume kuachana na tabia ya kutafuta vibanda hasara mara baada ya kupata fedha za mauzo ya tumbaku, pia litakuwa jambo la busara kukaa na familia zenu kupanga masula ya maendeleo,” alisisitiza Fatma.
Hata hivyo, DC huyo, pia aliwashauri wakulima hao wajenge utamaduni wa kujiunga na vyama vya kuweka na kukopa (Saccos) kama njia mbadala ya kulinda mapato yao yasichukuliwe na watu aliowaita ‘vibanda hasara’.
 
Fatma alisisitiza umuhimu wa wakulima hao kununua zana za kisasa za kilimo, hususan matrekta na waachane na kilimo cha jembe la mkono ambacho alidai hakina tija.

Akimkaribisha mkuu huyo wa wilaya kufungua soko hilo, Diwani wa Kata ya Mitundu (CCM), Charles Mongo alitumia fursa hiyo kupongeza kampuni za tumbaku zinazonunua zao hilo wilayani humo kwa misaada mbalimbali ya maendeleo ndani ya kata hiyo.

 

Leave a Comment