Iran kutofumbia macho haki yake ya kustafidi na nyuklia katika mazungumzo na kundi la 5+1


Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo hapa mjini Tehran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitofumbia macho haki yake ya kustafidi na teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani katika mazungumzo yajayo na kundi la 5+1 yatakayofanyika mjini Baghdad, Iraq. Sambamba na kubainisha kwamba nchi za Magharibi zinapaswa kutambua rasmi haki ya Iran ya kuwa na teknolojia nyuklia ili kujenga hali ya kuaminiana, Hujjatul-Islam Walmuslimin Kadhim Sidiqi amesema kuwa hakuna faida tena kutumiwa siasa za mabavu na vitisho ili kubadilisha msimamo wa taifa la Iran wa kustafidi na nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani.
Aidha amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijachoka kufanya kila jitihada kujenga imani kwa walimwengu ili kuwahakikishia kwamba shughuli zake za nyuklia ni kwa ajili ya malengo ya kiraia na kwamba hivi sasa inategemea kuwa Wamagharibi, nao pia wataithibitisha nia yao njema ili kufikiwa maelewano juu ya nukta za pamoja na kutatua matatizo yaliyopo.
Katika upande mwingine Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran ameashiria njama za Marekani, utawala wa Aal Khalifa na Aal Saudi za kuiunganisha Bahrain na Saudi Arabia na kusema kwamba mataifa ya eneo na hasa yale yenye kuipenda Bahrain na Waislamu wote duniani kamwe hayatokaa kimya kuhusiana na njama hiyo.

 

Leave a Comment