Sikika: Wabadhirifu fedha za umama wawajibishwe


Shirika la Sikika kimesema limesikitishwa na kushtushwa na ripoti ya iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyoibua matumizi mabaya ya fedha za umma na kiwango kikubwa cha misamaha ya kodi.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa misamaha ya kodi iliyotolewa imeongezeka kutoka Sh. bilioni 680.7 mwaka 2009/2010, hadi  Sh. trilioni 1.016 mwaka 2010/2011. Ongezeko hili ni sawa na 18% ya mapato yote yanayotakiwa kukusanywa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria, amesema hiki ni kiwango kikubwa ukilinganisha na nchi jirani za Kenya na Uganda na kwamba kibaya zaidi, misamaha hii imetolewa kwa watu wenye uwezo na makampuni makubwa ya kimataifa yenye mitaji mikubwa jambo linalolikosesha taifa mapato.

Alisema fedha zilizopotea kutokana na misamaha hii ya kodi, zingeweza kugharamia rasilimali watu katika mpango mkakati wa maendeleo ya sekta ya afya uliohitaji Sh. bilioni 500. 

“Huu ni mzaha mkubwa unaofanywa na Serikali, ukilinganisha na upotevu wa fedha uliotokana na misamaha hiyo ya kodi yenye utata,” alisema.

“Wakati upotevu huu wa mabilioni ya walipa kodi ukitokea nchini, bado nchi inakabiliwa na matatizo lukuki ya  upatikanaji wa huduma bora za jamii. Mathalan, kumekuwepo na upungufu wa rasilimali watu katika sekta ya afya, madawa, mfumo mbovu wa usambazaji wa madawa na vifaa tiba pamoja na uduni wa vifaa vya kutolea huduma za afya,” alisema.

Kiria alitoa wito kwa mamlaka husika kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na CAG na kuwawajibisha watendaji wa Serikali waliohusika na upotevu huo.

“Tunapongeza kazi kubwa na nzuri iliyo fanywa na CAG kwa kuibua ubadhilifu mkubwa wa fedha za umma uliofanywa na baadhi ya watumishi wa umma na taasisi za Serikali,” alisema Kiria.

CHANZO: NIPASHE

Leave a Comment