Makada zaidi waikimbia CCM


Na Waandishi wetu

20th April 2012

Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Nyampulukano (CCM) wilayani Sengerema, Hamis Mwagao (katikati) akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa anatangaza kujiunga Chadema jijini Mwanza jana. Kulia ni aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema na kushoto ni aliyekuwa Diwani wa CCM Kata ya Sombetini jijini Arusha, Alphonce Mawazo ambaye naye amekimbilia Chadema. (Picha na George Ramadhan).

Siku moja baada ya Diwani wa Kata ya Sombetini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha Alphonce Mawazo kujiengua katika chama hicho na kujiunga na Chadema, makada zaidi mkoani Arusha pamoja na Diwani mwingine wa CCM katika Kata ya Nyampulukano Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Hamisi Mwagao “Tabasamu” naye wametimkia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Diwani Mwagao alitangaza uamuzi wa kujiengua CCM na kujiunga Chadema jijini Mwanza jana katika mkutano na waandishi wa habari akiwa amefuatana na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema; Diwani aliyejiengua CCM Arusha, Mawazo pamoja na Katibu wa Chadema Kanda ya Dar es Salaam, Handry Kileo.

Akitangaza uamuzi huo, Mwagao alisema kwamba ameamua kujiuzulu nafasi ya udiwani kwa tiketi ya CCM baada ya kuona chama hicho hakina dalili yoyote ya kujirekebisha kutokana na kukabiliwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi.

Alisema amekuwa mstari mbele kupinga ufisadi na kuzungumzia matatizo yanayowakabili wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, lakini matokeo yake amejikuta akichukiwa na madiwani wenzake wa CCM pamoja na watendaji wa halmashauri hiyo.

Alidai kuwa kama zilivyo Halmashauri nyingi nchini, Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema pia inakabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa mabilioni ya fedha kama ilivyoainishwa katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Aidha, alidai kuwa Halmashauri ya wilaya hiyo imekuwa na maamuzi yasiyo ya kizalendo ikiwa ni pamoja na kuhujumu miradi ya maendeleo katika kata yake, hivyo ameona aachie ngazi na kujiunga na Chadema ambacho kimeonyesha dhamira ya kuwatumikia wananchi kwa dhati.

Akizungumzia hatua ya Diwani huyo, Lema ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema kwamba huu ndio wakati mwafaka kwa wana-CCM wasiokubaliana na sera mbovu za chama hicho tawala kujiengua na kujiunga Chadema.

Wanachama 2,402 kutoka vitongoji vitano vya Wilaya ya Ngorongoro,wakiwemo wenyeviti wa vitongoji vyao, jana walirudisha kadi za CCM kwa madai kuchoshw ana ubabaishaji wa viongozi wa chama hicho.

Katibu wa Chadema, Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alithibitisha kuwapokea wanachama jana na kufafanua kuwa baadhi ya viongozi waliohamia Chadema ndio waliokabidhiwa kadi za Chadema na kwamba wengine watakabidhiwa leo.

Aliwataja viongozi wa vitongoji waliorudisha kadi hizo kuwa ni Saitabau Tereto wa Kitongoji cha Enduleni katika Kijiji cha Esluway ambaye amehama na wanachama 478 na Mwenyekitw wa Kitongoji cha Ngiani, Kone Tema, ambaye amehama na wanachama 590.

Wengine ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngoyapase, Marko Mbeme ambaye amehama na wanachama 590; Mwenyekiti wa Kitongoji cha Embaruale, Saluni Meng’alana amehama na wanachama 224 na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Madukani, Robert Edward amehama na wanachama 520.

Golugwa alisema kuwa makada hao walisema kuwa wameamua kufuata nyayo za Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), James
Millya.

George Ramadhan, Mwanza na Cynthia Mwilolezi, Arusha

CHANZO: NIPASHE

Leave a Comment