Kiduchu wachaguliwa kidato cha tano


Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo

Wakati Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikitangaza nafasi za wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano, tathmini ya NIPASHE imegundua kuwa waliochaguliwa ni chini ya asilimia 10 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka jana.

Kati ya wanafunzi 426,314 waliofanya mtihani huo, 33,577 sawa na asilimia 9.98 walipata daraja la kwanza hadi la tatu, wakati watahiniwa 146,639 sawa na asilimia 43.60 walipata daraja la nne.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano ni wale waliofaulu daraja la kwanza, la pili na la tatu ambao masomo watakayokwenda kusoma (combination) wana alama zinazokubalika.

Mulugo alisema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule za serikali na vyuo vya ufundi ni 31,516 kati ya 180,216 (asilimia 17.5) ya waliofaulu mtihani huo wa Oktoba, mwaka jana na kupata daraja la kwanza hadi la nne.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, watahiniwa 148,700 hawajachaguliwa kujiunga na kidato cha tano wakati 563 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi.

Watahiniwa 156,089 sawa na asilimia 46.41 walifeli kabisa kwa kuambulia daraja sifuri.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mulugo alisema wanafunzi waliotimiza sifa zote za kujiunga kidato cha tano walikuwa 31,658.

Hata hivyo, alisema wanafunzi 142 kufaulu kwao hakukuweza kutengeneza maunganisho yoyote ya masomo na hivyo kukosa sifa za kuchaghuliwa.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuna punguzo la wanafunzi 4,850 sawa na asilimia 13.34  ya wanafunzi 36,366 waliochaguliwa mwaka juzi kujiunga na kidato cha tano kati ya 40,388 waliokusudiwa kipindi hicho.

Alisema wanafunzi waliochaguliwa mbali na kujiunga shule za sekondari za serikali, pia wamechaguliwa kujiunga katika vyuo vya ufundi.

Vyuo hivyo ni Arusha Technical College (ATC), Dar es Salaam Institute of Technology (DIT), Mbeya Institute of Science and Technology na Taasisi ya Maendeleo na Usimamizi wa Maji Dar es Salaam (WDM).

Mulugo alisema katika kipindi cha mwaka jana, wanafunzi waliopangwa kujiunga na kidato cha tano kwa masomo ya Sayansi walikuwa 16,493 sawa na asilimia 53.34.

Alisema hata hivyo, wanafunzi wavulana waliofanikiwa kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano kwa masomo ya Sayansi ni 12,282 sawa na asilimia 58.80 wakati wasichana waliochaguliwa ni 4,211 sawa na asilimia 45.13.

Aliongeza kuwa katika wasichana 9,481 waliokuwa na sifa zote za kupangwa kidato cha tano, wasichana 9,331 sawa na asilimia 98.42 ndiyo waliopangwa na wavulana walikuwa 22,177, lakini waliopangwa ni 21,622 sawa na asilimia 97.50 .

Alisema mbali na muunganisho wa masomo kuwa kikwazo cha kujiunga kidato cha tano, pia wapo waliopata daraja F katika muunganisho wa masomo ya kidato tano waliyoomba, huku wakiwa na umri zaidi ya miaka 25 wakati wa kumaliza kidato cha nne mwaka 2011 na wengine hawakutaka kupangwa katika shule za serikali na hivyo hawakujaza fomu (sel-form).

Naibu Waziri huyo alisema hali ya kupungua kwa wanafunzi wenye sifa ya kuchaguliwa kidato cha tano imesababisha shule nyingi na hasa zile zinazochukua wanafunzi wa masomo ya Arts, Biashara na Uchumi kutopata idadi waliyotaka ya wanafunzi.

Alisema serikali ilikuwa imetenga nafasi 15,00 za wasichana, lakini wamepatikana wasichana 9,378 tu wakati upande wa wavulana zilikuwa nafasi 26,000 waliopatikana ni 22,138 tu.

“Kwa kuwa mwaka huu tuna nafasi za kutosha, wanafunzi wote wenye sifa kupangwa katika machaguo mbalimbali ya masomo kidato cha tano,wizara inazielekeza Halmashauri wanaojenga shule au madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano walenge kukamilisha kazi hiyo kwa ajili ya kufungua madarasa hayo mwaka 2013,” alisema Mulugo.

1 Comment

  1. malulu joseph says:

    Note
    Educational system in tanzania particulary,makes learners to be slave of employment.not for self reliance.hey!,stakeholders can you focus far not infront?.

Leave a Comment