Trawu yaibua mapya Tazara


Chama cha Wafanyakazi wa Reli Nchini (Trawu), kimemtaka Waziri wa Uchukuzi Omari Nundu kutoyachukulia matatizo ya Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) kuwa ni ya kisiasa na kuwa ni mepesi, bali achukue mikakati zaidi kwa nia ya kuleta mabadiliko.

Aidha Trawu, imeitaka Serikali kuwafukuza kazi mara moja Mkurugenzi Mtendaji, Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Meneja wa Fedha, Meneja Mipango, Meneja wa Masoko, Meneja Ugavi, Mhandisi Mitambo, Meneja Usafirishaji pamoja na Meneja Teknohama na Habari kwa kile ilichodai kuwa wameshindwa kuiendesha Tazara kama kampuni.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Katibu wa chama hicho, Erasto Kihwele alisema kuwa Trawu kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya Waziri, aliyotoa  hivi karibuni kwa vyombo vya habari juu ya matatizo ya Tazara, ambayo yamekuwepo kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Kihwele alisema matatizo yote yalikabidhiwa kwa Waziri  huyo alipotembelea kwenye Ofisi za Shirika hilo Aprili 2011 na aliahidi kuwa angerudi Tazara ndani ya mwezi mmoja ili kuona mabadiliko na maendeleo, jambo ambalo hajalifanya kwa mwaka mmoja sasa wakati hali ya shirika hilo ikizidi kuwa mbaya.

Aliyataja baadhi ya matatizo ya shirika hilo kuwa ni pamoja na kutokulipwa kwa wakati mishahara ya wafanyakazi, shirika kushindwa kununua mafuta kwa ajili ya shughuli za kiuendeshaji, mizani mibovu, mikataba mibovu isiyo na tija, kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi NSSF, pamoja na kushindwa kulipa pensheni kwa wastaafu.

“Pamoja na maelezo mazuri ya Waziri, kwa vyombo vya habari, lakini hayaonyeshi ufumbuzi wa kudumu wa matatizo hayo, chama kinahesabu maelezo hayo kama zima moto, kitu ambacho hatukubaliani nacho,” alisema.

Kihwele aliongeza kuwa wafanyakazi wa Tazara wanataka mishahara yao kuanzia sasa ilipwe kwa ukamilifu ili michango ya Hifadhi ya jamii iweze kupelekwa kunakostahili na kwa wakati, hali itakayowawezesha wafanyakazi kupata mafao yao yanayotolewa na mifuko hiyo, kama vile matibabu, mazishi, uzazi na kuumia kazini.

Aidha Trawu imelitaka shirika hilo kusimamisha huduma ya usafiri wa treni kwa sababu za kiusalama.

1 Comment

  1. Enas says:

    Jamani walipeni wazee wa watu fedha zao, ni siku nyingi sana serikari imepuuzia, serikari ya zambia inanza kuwalipa je tanzania inakuaje, wazee mamestaafu siku nyingi sana hebu walipeni…

Leave a Comment