Nacte kufuta vyuo visivyo na sifa


Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), Dk. Primus Nkwera (kulia), akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.

st1\:*{behavior:url(#ieooui) } Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), limetangaza kuvisaka na kuvifungia vyuo vyote vinavyotoa mafunzo ya ngazi ya cheti na stashahada yasiyokidhi viwango vilivyowekwa na baraza hilo.

Vyuo hivyo vimo vinavyotoa mafunzo ya uandishi wa habari, ambapo Baraza hilo limesema kuanzia sasa hakuna chuo chochote kitakachopona kama kinatoa mafunzo kwa njia za ubabaishaji.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar ers Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Nacte, Dk. Primus Nkwera, alisema ili mafunzo ya chuo yaweze kutambulika ni lazima kiwe kimesajiliwa, kiwe na walimu wenye sifa pamoja kutumia mitaala inayotambuliwa na Baraza.

Aliwataka wazazi na wanafunzi wote wanaohitaji kupata elimu katika vyuo mbalimbali hapa nchini kuvichunguza kwanza kabla ya kujiunga navyo kwani wasipofanya hivyo watakuwa wanapoteza muda wao na fedha.

“Watanzania waulize kwanza chuo wanachotaka kusoma kama kimesajiliwa na mitaala gani kinayotumia kufundishia,” alisema Dk. Nkwera.

Kwa upande wa vyuo vinavyofundisha uandishi wa habari, Dk. Nkwera alisema Baraza limeanzisha mitaala mipya na kwamba kila chuo kinatakiwa kuifuta.

Alisema mchakato wa kupata mitaala ya uandishi wa habari ulifanywa kwa ushirikiano kati ya Nacte pamoja na Baraza la Habari Tanzaia (MCT).

Dk. Nkwera alisema hakuna sababu kwa Watanzania kuendelea kuibiwa kwa kusoma vyuo vya ubabaishaji ambapo mwisho wa siku vyeti watakavyopata havitatambulika popote.

Aliongeza kuwa mitaala mingine iliyotolewa ni ya Uuguzi katika vyuo mbalimbali na kwamba kama mtu anataka kusoma kwa uhakika awasiliane nao ili wampe orodha ya vyuo vyenye sifa.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema wakati wa kuwa na vyuo vya feki hususani katika taaluma ya uandishi wa habari umekwisha.

Alisema mitaala mipya ya uandishi wa habari inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika tasnia ya habari kwa kuwa imeandaliwa kwa uhakika.

1 Comment

  1. M.N. Sitta says:

    Dk. Primus Nkwera amejitahidi kutoa maelekezo kwa wadau wa vyuo. Lakini mi naona bado hajui wajibu wake wa kiutendaji. Mfano rahisi tu, mimi nataka kuanzisha chuo nitawezaje kupata maelezo husika kama WEBSITE yake ya NACTE haifanyi kazi kabisa. Katika dunia hii ya leo, information is power, inaonekana huyu jamaa halijui hilo. Dk. Primus Nkwera, fungua kwanza Website yako! Vinginevyo, utakuwa unajichora kwa kuongea na waandishi wa habari kana kwamba hujui kutumia internet.

Leave a Comment